Kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Parimatch imetangaza rasmi kuingia makubaliano ya kuidhamini klabu inayomilikiwa na Manispaa ya Jiji la Geita, Geita Gold ambayo inayoshiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2023/24.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Parimatch Tanzania, Erick Gerald wakati wa zoezi la utiaji sahihi wa mkataba ambao umefanyika leo katika ukumbi wa ofisi za Halmashauri ya Jiji la Geita baina ya Uongozi wa Kampuni hiyo mbele ya vyombo mbalimbali vya habari.
Aidha Erick amesema kandarasi wanayoingia na Geita Gold ni yenye faida kwa upande wa klabu katika kuelekea michuano ya ligi kuu inayotarajiwa kuanza siku chache zijazo na wamefungua milango ya ushirikiano na klabu na ligi zingine ambazo Parimatch inadhamini kimataifa.
“Mkataba huu ni mwaka mmoja baina yetu na Geita Gold lakini safari yetu haishii hapa Geita, tunaendelea kufanya mazungumzo ya hapa na pale na vilabu vingine vya ligi kuu na daraja la kwanza ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Shirikisho la Soko Tanzania (TFF) na bodi ya ligi ili kuhakikisha ligi ya Tanzania inakuwa na kwenda kimataifa”, amesisitiza Erick.
Kwa upande wake Katibu wa Klabu ya Geita Gold Simon Shija ameishukuru Kampuni ya Parimatch Tanzania kwa kuwaamini na kuwaunga mkono katika udhamini huo ambao utawasaidia kupunguza changamoto za uendeshaji wa klabu.
“Udhamini huo utatusaidia kurahisisha uendeshaji wa klabu na ushiriki wa mashindano mbalimbali pamoja na kuwa na tija kwa kuongeza thamani ya mpira wa miguu”, amesema Shija.