Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita Gold yaipeleka Azam machinjioni

Geita Vs Azam FC Geita Gold yaipeleka Azam machinjioni

Wed, 21 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Geita Gold leo inaikaribisha Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ikiwa uwanja wao wa nyumbani Nyankumbu, ambao wamekuwa na rekodi nao tamu ya kutopoteza mechi hata moja.

Geita iliyotoka kuadhibiwa na Simba mabao 5-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, inaikaribisha Azam ikiwa ni mara ya nne kukutana Ligi Kuu na imeshinda mchezo mmoja na sare mbili, msimu wa 2021 Azam (1-0), 2022 (2-2) na Agosti 2022 (1-1).

Wakati Geita Gold ikitambia rekodi hiyo ya kutofungwa na uwanja wao wa nyumbani, Azam chini ya Kocha Kali Ongala yenyewe inatambia rekodi ya kucheza michezo tisa bila ya kupoteza ikiambulia sare moja na ushindi michezo minane.

Akizungumza Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuirudisha timu kwenye hali ya ushindani huku akiweka wazi suala la rekodi ya kutofungwa halina nafasi.

“Rekodi zinaandikwa ili zivunjwe, hivyo tukiamini katika kutokufungwa matokeo yanaweza kubadilika, tumejiandaa kiushindani na tunahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo,” alisema na kuongeza;

“Nimeifanya kazi yangu kwenye uwanja wa mazoezi kwa kurekebisha mapungufu niliyoyaona kwenye mechi iliyopita, kilichobaki ni wachezaji wangu kufanya utekelezaji kwa kusaka ushindi dhidi ya Azam FC,” alisema.

Kwa upande wa Ongala alisema anaingia kwa kuwaheshimu wapinzani, anatambua ubora wao lakini na timu yake ni bora, hivyo anatarajia dakika 90 ngumu ambazo kila timu imejiandaa kusaka pointi tatu muhimu.

“Itakuwa ni mechi ya ushindani na nzuri kutokana na kila timu kuhitaji pointi kwenye mchezo huo, dakika 90 ndio zitakazoamua nani bora zaidi ya mwingine.”

Chanzo: Mwanaspoti