Kitendo cha Simba na Yanga kufuzu robo fainali ya michuano ya kimataifa ya CAF na kuipa nafasi Tanzania kuwakilishwa tena na timu nne msimu ujao, imeiongezea mzuka Geita Gold katika kupambana kwenye Ligi Kuu ili kumaliza nafasi za juu na kupata tiketi ya michuano hiyo.
Geita iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu baada ya kumaliza nafasi ya nne katika msimu uliopita wa Ligi Kuu, kwa sasa inahaha kuingia Nne Bora ikiwa imekusanya pointi 34 ikishika nafasi ya tano nyuma ya Azam na Singida Big Stars zilizopo juu yao nafasi ya tatu na ya nne.
Katibu Mtendaji wa Geita, Simon Shija alisema mafanikio ya Simba na Yanga yanatokana na uwekezaji uliofanywa na Mohamed Dewji na Gharib Mohamed wakitoa funzo kwa klabu nyingine nchini huku akitamba wameweka mikakati kuhakikisha wanakata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania.
“Klabu hizo zinasajili, kulipa mishahara mizuri kwa wakati, bonasi na kuweka kambi sehemu yoyote, hivyo inaleta motivation kwa wachezaji kufanya vizuri, kwetu klabu ndogo hili linatupa hamasa kubwa,” alisema Shija na kuongeza;
“Nasi tunatamani kupata udhamini kama huo tuweze kuwahudumia vizuri wachezaji wetu na tufike huko, Geita Gold tuna mikakati mizito kuhakikisha tunarudi msimu ujao tunamaliza kwenye nafasi nne za juu, nia tunayo wadhamini wetu wapo tayari na mazungumzo mbalimbali yanaendelea.”
Kipa wa Geita, Sebusebu Samson alisema mafanikio ya Simba na Yanga kufuzu robo fainali yanaipa heshima nchi na ligi yetu ambapo Geita Gold itaendelea kupambana kutopoteza nafasi iliyopo na kumaliza kwenye nafasi nzuri ili kuwakilisha kwenye nafasi hizo nne.
“Sisi kama timu tutapambana tusitoke kwenye nafasi tuliyopo, pili kupambana kwa nguvu zote kupigania nafasi nne za juu japo aliyepo juu yetu anatuzidi pointi nyingi lakini lolote linaweza kutokea kikubwa mapambano tu,” alisema Samson