Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita Gold mambo magumu Ligi Kuu, yatibuliwa Nyankumbu

Geita Gold Vs Tbatora.jpeg Geita Gold mambo magumu Ligi Kuu, yatibuliwa Nyankumbu

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mambo yameendelea kuwa magumu kwa Geita Gold na kumuweka kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleman ‘Morocco’ kwenye wakati mgumu baada yah ii leo kukosa tena ushindi katika uwanja wake wa nyumbani, Nyankumbu kwa kubanwa mbavu na Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo wa mzunguko wa tisa umepigwa leo Jumatatu Novemba 6, 2023 katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuanzia saa 10:00 jioni na kumalizika kwa suluhu (0-0) ukiwa ni mchezo wa nane mfululizo bila kuonja ushindi.

Huo ni mchezo wa tatu nyumbani kwa Geita Gold katika Uwanja wa Nyankumbu bila bila ushindi ikiambulia sare mbili na kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya KMC. Pia ni mchezo wan ne nyumbani ukiwemo dhidi ya Yanga uliochezwa CCM Kirumba, Mwanza bila ushindi.

Sare hiyo tasa ni ya pili mfululizo kwa Geita Gold baada ya mchezo uliopita kumaliza 0-0 ugenini dhidi ya Tanzania Prisons, huku ikiwa sare tasa ya tatu msimu huu ikiwemo ya ugenini dhidi ya Mashujaa FC.

Matokeo hayo yasiyo ya kuridhisha ni mfululizo wa matokeo mabaya kwa Geita Gold msimu huu, ambapo imecheza nane mfululizo bila ushindi katika mechi zake tisa msimu huu, ambapo imeshinda mechi moja dhidi ya Ihefu (1-0), sare nne na kupoteza nne, ikikamata nafasi ya 15 na pointi zao saba.

Kocha wa Geita Gold, Hemed Suleman ‘Morocco’ ameendelea kuwapangua makipa wake, ambapo leo amempa tena nafasi kipa, Constatine Malimi ambaye alidaka mchezo uliopita ugenini dhidi ya Tanzania Prisons na kufanikiwa kuondoka na cleensheet katika michezo yote miwili.

Makipa wengine wa timu hiyo, Erick Johora ambaye alianza vizuri msimu akidaka mechi nne mfululizo alipumzishwa katika mchezo dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar kabla ya kurudi langoni kwenye sare ya 2-2 na Dodoma Jiji, huku Sebusebu Samson akidaka mechi mbili ambazo timu hiyo ilipoteza kwa mabao mengi dhidi ya Yanga (3-0) na Mtibwa Sugar (3-1).

Kipa wa Tabora United, John Noble, raia wa Nigeria amekuwa na kiwango kizuri tangu atue klabuni hapo msimu huu akiwa na cleensheet tano katika michezo nane, huku akiruhusu mabao matatu pekee.

Hadi sasa hakuna mchezaji yeyote wa Geita Gold aliyefunga mabao zaidi ya moja, ambapo mpaka sasa mabao matano ya timu hiyo yamefungwa na Elias Maguli, Valentino Mashaka, Mahamud Hassan na Tariq Kiakala.

Tabora United bado haijaonja ushindi katika michezo ya ugenini msimu huu, ikiambulia sare sare nne dhidi ya Kagera Sugar, Singida Fountain Gate, Coastal Union na Geita Gold huku ikipoteza miwili mbele ya JKT Tanzania na Azam FC zote kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Katika sare hizo nne za ugenini timu hiyo haikuruhusu bao.

Geita Gold inakamata nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikivuna pointi saba ikifunga mabao matano na kuruhusu 11, huku Tabora United ikikamata nafasi ya nane ikiwa na pointi 11 katika michezo tisa.

Geita Gold: Constatine Malimi, Steven Mgaju, Antony Mligo, Mahamud Hassan, Erick Kyaruzi, Samwel Onditi, Godfrey Julius, Raymond Masota, Tariq Kiakala, Valentino Mashaka na Offen Chikola.

Tabora United: John Noble, Shaffih Maulid, Said Mbatty, Andy Bikoko, Haritier Lulihoshi, Paulin Kisindi, Najim Ibrahim, Lambele Jerome, John Nakibinge, Abbas Athuman na Jackson Mbombo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: