Wakati mabao 29 yakifungwa kwa penalti, timu za Geita Gold na Prisons ndizo zimeonekana kunufaika zaidi, huku Dodoma Jiji, Yanga na Ruvu Shooting zikiathirika pakubwa.
Jumla ya penalti 43 zimepatikana kwenye mechi 23 zilizochezwa hadi sasa kwa baadhi ya timu, huku mabao 29 yakifungwa na 14 yakikoswa na timu hizo.
Hata hivyo licha ya idadi hiyo kubwa ya penalti, Mtibwa Sugar imekuwa timu pekee ambayo haijafunga wala kukosa bao lolote la penati katika mechi zote ilizocheza.
Prisons na Dodoma Jiji ndizo zimepata penalti nyingi (tano kila timu), ambapo Wajelajela wamefunga nne na kukosa moja, huku wenzao wakikosa nne na kupatia moja.
Geita Gold wao wamepata penalti nne na kufunga zote, huku Simba iliyopata tatu na kuzitumia vyema zote sawa na KMC na Coastal Union, huku Yanga wakikosa mbili kati ya tatu walizopata kama ilivyo kwa Ruvu Shooting.
Kwa upande wa Azam wamefunga penalti mbili kati ya tatu, Singida BS wakifunga tatu kati ya nne ilizopata, huku Mbeya City, Namungo na Ihefu wao katika penalti mbili walizopata, kila timu imenufaika na bao moja.
Polisi Tanzania ambao wanaburuza mkia kwa pointi 16 wamefunga penalti moja waliyoipata, huku Kagera Sugar wakikosa moja hiyo hiyo waliyoipata.