Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Garnacho ni balaa jingine Man United

Skysports Alejandro Garnacho 6074607 Garnacho ni balaa jingine Man United

Wed, 8 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Japokuwa bado ana umri mdogo lakini taratibu ameanza kugeuka kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu ya Manchester United kutokana na kasi yake, kufunga sambamba na kutoa pasi za mabao.

Tayari ameshaanza kuipata imani ya kocha Eric ten Hag ambaye amekuwa akimpa nafasi kila wikiendi akimchezesha kwa dakika nyingi kwa kadri mechi zinavyozidi kwenda.

Huyo ni Alejandro Garnacho. Winga chipukizi wa Man United ambaye kwa muda mfupi tu amekuwa miongoni mwa watu muhimu ndani ya timu hiyo licha ya kwamba ni mdogo kwenye suala zima la umri.

Garnacho kwa sasa ndiyo kwanza ana miaka 18 lakini anapokuwa uwanjani unaweza kushangazwa na kile anachokifanya akiwa na uwezo wa juu wa kupambana na mabeki ambao wengine wamemzidi umri na umbo.

Ndani ya kikosi cha Man United, Garnacho amekuwa akitumiza zaidi kama winga wa kushoto ambapo amekuwa na faida napo kutokana na matumizi ya mguu wa kulia licha ya kwamba anaweza kutumia miguu yote kwa usahihi.

Kasi, usahihi wa pasi, kukimbia na mpira mguuni na kutoa pasi za mabao ni miongoni mwa sifa ambazo zimekuwa zikimbeba winga huyo na amekuwa akivionyesha hivyo kila mara anapopata nafasi.

Kocha wa Man United, Ten Hag amekuwa akimtumia Garnacho kama silaha yake ya kupata mabao pale ambapo anapokuwa anaona mabeki wa timu pinzani wamechoka na hawawezi kupambana kwa nguvu zaidi.

Ten Hag anamtumia hivyo kwa kuwa amekuwa akifaidika na kasi ya winga huyo ambapo mabeki wamekuwa wakishindwa kumzuia kirahisi na mwisho hujikuta wakimchezea faulo ambazo zinawanufaisha kikosi hicho.

Winga huyo licha ya kuichezea Man United lakini alizaliwa kwenye jiji la Madrid kwa wazazi wenye uraia wa Argentina na tayari ameshachagua kuichezea timu ya taifa bya Argentina mbele ya Hispania ambapo alizaliwa.

Licha ya kwamba yeye ni mzaliwa wa Argentina ambapo anatokea nyota bora wa soka, Lionel Messi lakini Garnacho, ni shabiki mkubwa wa mpinzani wa Messi, Cristiano Ronaldo na mahaba yake kwa Mreno huyo yapo waziwazi.

Garnacho ameshaonyesha kwa namna gani anamzimikia Ronaldo ambapo mara kadhaa anapofunga mabao amekuwa akishangilia kwa baadhi ya staili maarufu za Ronaldo ikiwemo ile ya Siuuuu.

Hadi sasa winga huyo ameshacheza mechi 13 za Premier, akichangia mabao manne ndani ya kikosi hicho, akifunga mabao mawili na kutoa asisti mbili.

Winga huyo licha ya kuchezewa faulo mara kadhaa na wapinzani wake lakini amekuwa na nidhamu ya hali ya juu kwani kwenye mechi hizo 13 alizocheza ameonyeshwa kadi mbili pekee za njano huku akiwa hana kadi yoyote nyekundu.

Kutokana na umri wake na udogo wake ndiyo kumemfanya akose muda mwingi wa kucheza akiwa ametumika kwenye dakika 397 ndani ya timu hiyo kwenye mechi za Premier.

Kando ya kucheza kwenye Premier, winga huyo pia ametumika kwenye kombe la Europa League akiwa amecheza mechi sita akifunga bao moja na akitumia dakika 212.

Pia winga huyo alikuwa mtu muhimu wa Man United kwenye Kombe la Carabao ambalo walilitwaa wiki mbili nyuma kwa kutoa asisti mbili katika mechi tano alizocheza, na akipata nafasi ya kucheza kwenye Kombe la FA ambapo amecheza mechi tatu akifunga bao moja kama ilivyo kwa asisti huku akitumia dakika 131.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: