Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi na siri ya kipigo, Robertinho kikaangoni

Gamondi Yanga Yake Gamondi na siri ya kipigo, Robertinho kikaangoni

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati kocha Miguel Gamondi akifichua siri ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Simba, mwenzake Roberto Oliveira 'Robertinho' anatajwa kukalia kuti kavu kutokana na matokeo hayo ya mechi iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Maba mawili ya Maxi Nzengeli na mengine matatu yaliyofungwa na Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Stephane Aziz Ki, yalitosha kuipa Yanga ushindi huo mnono ambao umeipeleka kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 21.

Akizungumzia matokeo hayo, Gamondi alisema kuwa hayakupatikana kwa bahati mbaya kwani timu yake ilijiandaa kuyapata kutokana na namna walivyofanyia kazi ubora na udhaifu wao na ule wa Simba.

"Unajua soka ni mchezo wa maandalizi, ulichokiona uwanjani tulikifanya sana mazoezini kwetu na hapa tulikuja kuburudika.

"Tulitarajia kushinda kwa sasababu tulijianda vyema na nilisema hivi hata kabla ya mechi," alisema Gamondi.

Kocha huyo alisema kuwa aliamini kutawala eneo la kiungo kungekuwa silaha kubwa kwao kuimaliza Simba na ndilo jambo lililotokea, akiwasifu viungo wake hasa Pacome, Nzengeli na Aziz Ki ambao waliipoteza safu ya kiungo ya wapinzani wao.

"Niliisoma vyema Simba na kujua ubora wao na mapungufu, wako vizuri kwenye eneo la kiungo na sisi tuna watu bora eneo hilo.

"Nawaamini wachezaji wangu, niliwaambia wasiwe na presha bali wafanye kile wanachofanya kila siku mazoezini na hata kwenye mechi na nafurahi walinielewa na kufanya hivyo, najivunia wao," alisema Gamondi.

Gamondi alisema kuwa kwa sasa nguvu na akili zao wanazielekeza katika mchezo dhidi ya Coastal Union, kesho Jumatano katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Wakati Gamondi akitambia safu yake ya kiungo, hali inaonekana kuwa ngumu kwa Robertinho ambaye amejikuta katika presha ya kupoteza kibarua chake baada ya kichapo cha juzi.

Inaripotiwa kuwa baada ya mchezo wa juzi, kundi kubwa la viongozi wenye ushawishi ndani ya Simba wakiwemo wale ambao awali walikuwa wanamuunga mkono Robertinho, linaonekana kupoteza imani naye na linatoa ushauri kuwa awekwe kando.

"Kuhusu uamuzi wa kumtimua bado haujafanywa na wala hatujakaa kuzungumzia hilo kama inavyoandikwa mitandaoni. Tumeona tuwe watulivu kwa sasa ili tusifanye uamuzi wa presha lakini kiuhalisia nafasi ya kocha kubakia ni finyu," alisema mmoja wa viongozi wa Simba.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: