Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi kuisapraizi Belouizdad

Gamondi Yanga Yake Gamondi kuisapraizi Belouizdad

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga wajanja sana. Baada ya kugundua wapinzani wake kwenye mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi, CR Belouizdad kutoka Algeria wanawafuatilia kwa karibu, benchi la ufundi la ‘Wananchi’, chini ya kocha Muargentina, Miguel Gamondi limeamua kuandaa sapraizi matata itakayowamaliza waarabu hao.

Yanga kupitia mashushushu wake iliyowaweka Algeria, imebaini Belouizdad wameshtukia ubora wa Yanga na kuanza kuufanyia kazi ili kuwadhibiti, lakini kocha huyo na kikosi kwa ujumla wameamua kuingia kivingine jambo ambalo hakuna anayelitabiri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema anajua wazi wapinzani wake hao wanaifuatilia kwa makini Yanga, hivyo hawezi kuishi kwa mazoea na sasa anaanda timu itakayowashangaza wengi.

Kocha huyo aliyeshinda mechi nane kati ya tisa za ligi msimu huu, alisema anaiheshimu Belouizdad na kwenye mechi baina yao itakayopigwa Novemba 24, mwaka huu nchini Algeria ataingia katika namna tofauti.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kazi kubwa waliyofanya hadi kufika sasa, hakika wanastahili pongezi. Siku zote ukifanya vizuri lazima mpinzani unayeenda kukutana naye aangalie ubora na udhaifu wako, na CR Belouizdad naamini wanafanya jambo hilo, hivyo naandaa timu kwa namna ya tofauti, lengo ikiwa ni kupata matokeo tunayoyahitaji.

Yawezekana kukawa na mabadiliko kwenye kikosi chetu, lakini yote hayo tutayajua na kuyapitisha katika mazoezi ya mwisho,” alisema Gamondi.

Hata hivyo, Mwanaspoti kutokana na mazoezi ya Yanga yanayoendelea, linajua huenda kikosi kikawa na mabadiliko kwenye eneo lake la ushambuliaji katika mechi na Belouizdad.

Kocha na mchambuzi wa soka nchini, Kenny Mwaisabula alisema Yanga itahitaji mabadiliko kutokana na namna benchi la ufundi linataka kucheza kwani mechi za kimataifa mara nyingi hazizoeleki.

“Kwa sasa kocha ndiye anakuwa na uamuzi wa kupanga timu yake. Huenda akaona kuna sehemu timu yake inahitaji mabadiliko ya wachezaji au mchezaji kutokana na namna alivyowasoma wapinzani.

“Mara nyingi mechi hizi za kimataifa zinakuwa na mipango tofauti na zile za ligi, hivyo tusishangae kuona mabadiliko ya wachezaji au mfumo kwani ni mchezo tofauti na mahitaji yake ni tofauti na mechi zilizopita,” alisema Mwaisabula.

Yanga inatarajia kusafiri kwenda Algeria kwaajili ya mechi hiyo, Novemba 22, ambako itaenda na kundi la wachezaji walioko kambini na wale walio katika timu ya taifa ya Tanzania, huku wengine, Djigui Diarra, Khalid Aucho na Stephane Aziz Ki wakitarajiwa kujiunga na timu juu kwa juu nchini Algeria.

Chanzo: Mwanaspoti