Sahau kuhusu kiwango kilichoonyeshwa na Yanga katika mechi za mashindano, ikiupiga mwingi na kutembeza bolu uwanjani ikigawa dozi nene kwa wapinzani, kikosi cha timu hiyo kinaendelea kujifua, huku Kocha Miguel Gamondi akiwakomalia mastaa wote ambao hawakuitwa timu za taifa.
Kocha huyo na mastaa hao wapo chimbo kambini, Avic Town, Kigamboni baada ya kutoka kuiongoza timu hiyo kwenye jumla ya mechi sita za mashindano ikigawa dozi za mabao 15 kwenye michezo mitatu ya mwisho iliyopita, akijiandaa mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merrikh ya Sudan.
Licha ya kutokuwepo kwa mastaa 11 wa timu hiyo walioitwa kwenye timu za taifa, zinazojiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast, wengi wao wakiwa wa kikosi cha kwanza, lakini kocha huyo ametahadharisha kwamba hadi sasa hakuna mwenye uhakika wa namba kikosini.
Alisema hiyo inatokana na ushindani uliopo kwa wachezaji wa timu hiyo na sasa yupo kambini akiendelea kusuka timu hiyo kwa wachezaji waliopo huenda wakampa mfumo mpya ambao hajawahi kuutumia katika mechi saba zilizopita zikiwamo sita za mashindano na moja ya kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs ya Sauzi.
“Pamoja na timu kupata matokeo mazuri kwenye michezo tuliyocheza hadi sasa bado sijapata wachezaji wa kikosi cha kwanza kutokana na nafasi za wachezaji nilionao kila mmoja kuonyesha uwezo na kuhitaji kucheza kwenye kikosi hicho, hivyo Yanga kila mmoja ana nafasi ya kucheza kulingana na timu tunayokutana nao,” alisema Gamondi.
Mastaa wa Yanga walioitwa timu za taifa ni; Metacha Mnata, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Bakar Mwamnyeto, Dickson Job, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Jonas Mkude, Djigui Diarra, Stephane Aziz Ki, Khalid Aucho, Gift Fred ambao kati yao, Diarra, Job, Mwamnyeto, Aucho, Aziz Ki na Mzize walikuwa wameanza kujipata ndani ya kikosi cha Gamondi.
Gamondi, aliwapa mastaa wake mapumziko ya siku moja na juzi walirejea kambini kwa ajili ua kuendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El-Merrikh ya Sudan, mchezo utakaopigwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Pele (zamani Nyamirambo) jijini Kigali, Rwanda baada ya mipango ya Wasudani kuupeleka Morocco kukwama.
“Hakuna sababu ya kupumzika, tayari tulipumzika siku moja, tumerejea mazoezini, tunatakiwa kufikia malengo, hivyo ni vyema tukaongeza nguvu katika kipindi hiki kuhakikisha tunafikia malengo yetu,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Wachezaji wanatambua ugumu katika michuano ya kimataifa na ligi kuhakikisha tunafikia malengo kutetea mataji mawili ya ndani na kufika hatua nzuri kimataifa, hivyo utimamu ni muhimu zaidi tutaendelea tulipoishia na waliopo lengo ni kuhakikisha kila mchezaji anaingia kwenye mfumo na kufanya kile ninachokihitaji.”
Yanga itacheza na El Marreikh baada ya kuitoa Asas FC ya Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1 katika mchezo wa hatua ya awali, michezo yote ilichezwa katika Uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar.