Katika kuhakikisha timu yake haipoi, Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi, ameelekeza kikosi chake kiendelee na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa kuwakabili wapinzani wao kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al-Merrikh ya Sudan, imeelezwa.
Badala yake kocha huyo alitoa mapumziko ya siku moja na tayari wachezaji wa timu hiyo wameingia kambini kuendelea na maandalizi.
Yanga imeanza msimu huu kutoa vipigo vizito katika Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, michuano hiyo ikisimama kupisha kalenda ya kimataifa.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watarejea tena dimbani ugenini Septemba 16, mwaka huu huko wakianzia ugenini na mchezo wa marudiano utafanyika Septernba 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinasema Gamondi amegomea wachezaji kwenda mapumziko katika kipindi hiki akisema wanaratiba ngumu mbele yao.
“Awali tulitarajia timu itakuwa na mapumziko, lakini Gamondi akasitisha, ametoa siku moja pekee ya kupumzika na baadae amewataka wachezaji warejee kambini kuendelea na programu kwa nyota wote ambao hawajaitwa katika vikosi vya timu za taifa, anataka kasi waliyokuwa nayo iendelee watakapoikabili Al-Merrikh,” Kimeeleza chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Gamondi amesema anaamini ana kikosi bora chenye uwezo wa kupata matokeo katika mchezo wowote lakini hataki kuona wachezaji wanaenda mapumziko kwa sasa kwa sababu ya mashindano yaliyoko mbele yao.
“Hakuna sababu ya kupumzika, tulipumzika siku moja na tayari tumerejea uwanjani, tunatakiwa kufikia malengo yetu, hivyo ni vyema tukaongeza nguvu katika kipindi hiki kuhakikisha tunafikia tunapohitaji,” amesema Gamondi.
Ameongeza Al-Merrikh ni timu nzuri ina wachezaji ambao wanaweza kupata matokeo, hivyo hakuna umuhimu wachezaji kupumzika wakati wanahitaji kucheza hatua ya makundi.
“Young Africans haijawahi kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tunahitaji kutumia mapumziko ya Ligi Kuu kwa ajili ya kuendelea kutengeneza timu na kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mechi zilizopita, ikiwamo kuruhusu bao au kusababisha Penati,” Gamondi amesema.
Young Africans imesonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuwaondoa ASAS FC ya Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1, michezo yote miwili ikichezwa kwenye Uwanja wa Azam, kufuatia wapinzani wao kutokuwa na Uwanja wa nyumbani wenye viwango kwa sasa.
Msimu uliopita Young Africans ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya mabingwa USM Alger ya Algeria lakini ikakosa taji kwa faida ya mabao ya Ugenini waliyofunga Waarabu hao.