Baada ya kuishuhudia Yanga katika mechi tatu za ushindani, kuna mabadiliko ya kiuchezaji kati ya sasa na ilivyokuwa msimu uliopita chini ya kocha Nasreddine Nabi.
Kama ni kwenye ujenzi, Nabi alitengeneza msingi, sasa Miguel Gamondi anakamilisha ujenzi wa nyumba.
Katika misimu ya karibuni kwenye soka la Tanzania, haijawahi kushuhudiwa timu inayocheza soka la kushambulia katika kiwango ambacho Yanga wanafanya.
Kigezo cha kwanza ambacho Gamondi anatumia pale anapopanga kikosi chake, lazima mchezaji uwe fit na tayari kukimbia sana uwanjani.
Kwa aina hii ya uchezaji ipo siku kuna timu itashushiwa mzigo wa magoli. Yanga ya Gamondi ni marufuku kwa timu pinzani kumiliki mpira hata kwa sekunde 30.
Timu inapopoteza mpira utaona wachezaji wanavyohaha kuurudisha kwenye himaya yao haraka. Kwa aina ya 'intensity' ambayo Yanga wanacheza nayo, ni timu chache sana ambazo zinaweza kuhimili kwa dakika zote 90.
Jambo pekee ambalo Gamondi anahitaji kulifanyia kazi ni umaliziaji. Kama Yanga itatumia angalau nusu ya nafasi wanazotengeneza basi kila mechi watakuwa wakiondoka na ushindi mnono.
Tumezoea timu nyingi huanza mchezo taratibu na kumaliza kwa kasi au kuwa na vipindi vya umiliki wa mchezo lakini ni tofauti kwa Yanga. Inavyoanza ndio hivyo hivyo itakavyomaliza.
Katika mchezo dhidi ya Asas Fc, zilifika nyakati Asas licha ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0, walilazimika kujiangusha, kupoza mashambulizi na kupoteza muda maana sio kwa 'moto' waliokuwa nao.