Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi hajaridhika na bao 4 dhidi ya Vital’O, amtaja Chama

Sac Gamondi Chama Dube Aziz Clatous Chama na Gamondi

Mon, 19 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga SC imeshinda mabao 4-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kitu cha kushangaza ni kocha mkuu, Miguel Gamondi amewaka kutokana mastaa wa timu hiyo kukosa umakini katika kutumia nafasi, akisema wenyeji wa mechi hiyo walistahili kupigwa bao nyingi.

Yanga ilipata ushindi huyo kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambao Vital’O iliutumia kama wa nyumbani, ikishuhudiwa Prince Dube, Clatous Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz KI kila moja akifunga bao, lakini Gamondi licha ya kuwapongeza wachezaji, lakini amewageukia na kuwaambia; “Kama tuna uwezo wa kushinda zaidi tushinde, tunatakiwa kutumia nafasi zaidi sio kama tulichofanya leo.”

Akizungumzia zaidi kauli hiyo, Gamondi alisema licha ya timu kushinda 4-0 lakini bado wangeweza kupata ushindi mkubwa zaidi endapo wangetulia na kutumia nafasi walizotengeneza katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gamondi alisema hataki kuwa kocha wa kuridhika na matokeo madogo kwa kuwa hilo linaweza kushusha viwango vya wachezaji anaoamini wanaweza kufanya vizuri zaidi.

“Hizi ni mechi ambazo wakati mwingine zinaweza kuamuliwa kwa kuangalia ulifungwa ngapi na wewe ulifunga mangapi, kama tunaweza kutengeneza nafasi basi tunatakiwa kuzitumia kwa wingi,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Tunawaheshimu wapinzani wetu (Vital’O), lakini tulikuwa na uwezo wa kushinda kwa idadi kubwa zaidi ya hiki tulichofanya jana (juzi), mimi sio kocha ninayependa kuridhika na matokeo madogo, tukifanya kosa kama hili linaweza kutupunguzia ubora wa wachezaji.”

Kocha huyo ameongeza kuwa bado Yanga haijafuzu raundi ya pili hadi itakapoitoa Vital’O, akisisitiza baada ya mapumziko ya siku moja watarudi mazoezini kujipanga kwa mechi ya marudiano alioutabiri kuwa mgumu.

“Bado hatujafuzu, hizi ni dakika 90 za kwanza nani anajua kipi kitatokea katika mchezo wa marudiano, tutapumzika kwa siku moja au mbili baada ya hapo tutarudi kujipanga kwa mechi hiyo,” alisisitiza Gamondi.

Yanga itarudiana na Vital’O Jumamosi ijayo, huku ikihitaji ushindi au sare tu ili kusonga hatua inayofuata ambapo itakutana na mshindi kati ya SC Villa ya Uganda iliyochapwa nyumbani juzi kwa mabao 2-1 na Commercial Bank ya Ethiopia.

AMTAJA CHAMA

Katika hatua nyingine kocha Gamondi amesifu kiwango kilichoonyeshwa na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama aliyeanza katika kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza tangu aliposajiliwa kutoka Simba katika mchezo huo dhidi ya Vital’O ya Burundi na kuasisti na kufunga bao wakati Yanga ikishinda 4-0.

Kocha huyo alisema, Chama ni mchezaji mzuri na mzoefu wa michuano ya Afrika hivyo, licha ya presha kubwa iliyopo juu ya kumtumia mara kwa mara mchezaji huyo, anachozingatia ni weledi.

“Kila mchezaji hapa ana nafasi sawa na wengine ya kucheza kikosi cha kwanza kwa sababu tuna wachezaji bora katika maeneo yote uwanjani na hiki ndicho kiwango ambacho tumekitengeneza kwenye timu iwe ni kwa kipindi kirefu au kifupi,” alisema Gamondi.

Gamondi aliongeza, mashabiki watarajie makubwa kwa mchezaji huyo huku akisisitiza uwepo wake ndani ya kikosi cha Yanga ni muhimu kutokana na mahitaji ya timu hiyo, ambayo malengo yake ni kushinda mataji mbalimbali inayoshiriki msimu huu.

Katika mechi hiyo Chama alimtengenezea nafasi Dube kwa kisigino kabla ya kufunga bao la pili kipindi cha pili na Mzize kuongeza la tatu na Aziz Ki akafunga kwa penalti dakika za lala salama na kumfanya Mzambia huyo kuendeleza rekodi katika mechi za CAF, kwani akiwa na Simba aliiwezesha kutinga robo fainali mara tano, akifunga mabao 15 na kuasisti sita katika mechi 44 alizoichezea tangu ametua kikosini hapo.

Chama alijiunga na Simba Julai Mosi, 2018, baada ya kuachana na Lusaka Dynamos ya kwao Zambia na msimu uliopita katika makundi alifunga bao moja na kuasisti moja Simba ikitolewa na Al Ahly ya Misri.

Rekodi nzuri kwake katika Ligi Kuu Bara ni za msimu wa 2022/2023 alipohusika katika mabao 18.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live