Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi awatumia ujumbe kina Chama

Gamondi Chama Dube Abuya 91021 Wachezaji wa Yanga, Chama, Aziz Ki na Pacome.

Tue, 16 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amefichua kuwa katika falsafa yake ya mpira anapenda zaidi wachezaji wapambanaji wenye uwezo wa kushambulia na kukaba kwa wakati mmoja, huku akiendelea kusisitiza kuwa hatompanga mchezaji kwa sababu ya jina lake, bali kile anachokionyesha uwanjani.

Katika dirisha hili kubwa, Yanga imewasajili wachezaji kadhaa akiwamo, Clatous Chama kutoka Simba, Prince Dube akitokea Azam FC, Aziz Andambwile (Singida Fountain Gate), golikipa Khomeiny Aboubakar na Duke Abuya (wote kutoka, Singida Black Stars), na Chadrack Boka kutoka FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya timu hiyo, kocha huyo alisema yeye ni raia wa Argentina, lakini ana asili ya Italia, ambapo nchi zote hizo hupenda kucheza soka safi, lakini wana asilia ya upambanaji na kucheza kwa 'jihadi' kwa ajili ya kusaka ushindi.

"Msimu uliopita tulicheza vema, tulifunga mabao mengi na kushinda michezo mingi, msimu huu tumesajili wachezaji wengine wazuri na bora, kwangu mimi naona vizuri kwa sababu watapambana mazoezini ili kunionyesha ubora wao, ila nidhamu ndiyo ufunguo wa mafanikio, kwangu mimi nataka kuona kila mchezaji anapambana kupata namba.

"Mimi siangalii jina la mtu, hili narudia tena na tena, naangalia anafanya nini uwanjani, anaweza kuletwa mchezaji mwenye jina kubwa, lakini linatakiwa jina hilo lifanye kitu ndani uwanja, watu wanaweza kusema kocha ana machaguo mengi sana, lakini anachoangalia ni kikosi chake cha kwanza kinachompa matokeo bora," alisema Gamondi.

Kuhusu falsafa ya soka lake alisema yeye binafsi anapenda sana wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kujitoa na kupambana kwa ajili ya timu.

"Mimi nimetoka Argentina, lakini nina asili ya Italia, hivyo sisi pamoja na kucheza soka safi lakini ni wapambanaji, napenda kuona wachezaji wangu wakipambana, yaani kama kufa ufie uwanjani ukiipigania nembo, na hicho nimeshaonyesha msimu uliopita," alisema.

Aliongeza, "ukiangalia baadhi ya mechi zetu za ligi tulikuwa tunapata ushindi dakika za mwisho kabisa, angalia tulivyocheza dhidi ya Al Ahly, CR Belouizdad na Mamelodi Sundowns, tulifanikiwa zaidi kwa sababu ya kupambana na hiyo ndiyo falsafa yangu ya mpira, yaani wote tunashambulia na wote tunakaba," alisema Gamondi.

Akizungumzia mechi ya Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chiefs itakayochezwa, Julai 28, mwaka huu, nchini Afrika Kusini, alisema haitokuwa kipaumbele sana kwake, badala yake ataitumia kuangalia ubora na ufiti wa wachezaji wake, wakiwamo wachezaji wapya, ili ajue pa kuanzia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: