Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amewataka mastaa wake kuelekea dabi kupunguza presha na wacheze soka la kushambulia na kuzuia ili kuweza kuipa timu matokeo mazuri ndani ya dakika 90.
Gamondi amefunguka hayo baada ya kuitazama Simba kwa dakika 180 dhidi ya Ihefu wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kwenye Super League dhidi ya Al-Ahly wakitoka sare ya bao 2-2.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema anatambua utakuwa ni mchezo mgumu na wa ushindani, hivyo amewaandaa wachezaji wake kisaikolojia kuhakikisha wanatumia dakika 90 vyema kupata matokeo.
“Ni dabi ambayo imekuwa ikifanyika kila msimu, hivyo kwa kuwa nina wachezaji wengi ambao wameshaizoea nimewaandaa kucheza kwa kuwaheshimu mpinzani lakini pia kucheza mchezo waliouzoea wa kushambulia na kukaba.
“Sio rahisi lakini inawezekana kutokana na namna nilivyokaa na kikosi changu na kuweka mipango.Nimewaangalia Simba kwa dakika 180 hivyo nimeona ubora na upungufu wao,” alisema Gamondi.
Alisema hadi sasa hana majeruhi yeyote anakiandaa kikosi kikiwa kamili hivyo anaamini dakika 90 zitaamua nani bora huku akisisitiza hawezi kurudia makosa aliyoyafanya kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ametaja sababu iliyowatoa kuwa ni penalti ambazo hazina mwenyewe lakini kimpira timu yake ilicheza vyema.
“Kwenye mchezo ule ambao tulipoteza kwa penalti timu yangu ilikuwa bora shida ilikuwa ni kukosa umakini kwenye umaliziaji tatizo ambalo silitarajii kwenye mchezo wa Jumapili kutokana na maandalizi niliyofanya na namna timu imeandaliwa kucheza,” alisema.
DAKIKA 180 ZA SIMBA
Kwenye dakika 180 alizozishuhudia Gamondi kwa Simba imefunga mabao manne ikifungwa mabao matatu ilitoka 2-2 na Al Ahly na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC.
Kwenye mechi hizo mbili Simba ilifungwa kipindi cha kwanza mabao mawili moja dhidi ya Al Ahly na lingine dhidi ya Ihefu wakati ilifunga bao moja dakika za kwanza mengine matatu kipindi cha pili. Wakati Gamondi akifuatilia ubora na upungufu wa Simba alicheza mechi mbili na kushinda zote akifunga mabao matano na kuruhusu mabao mawili. Alianza na Azam FC 3-2 na 2-0 dhidi ya Singida Big Stars.