Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi ataka Yanga kufuzu kwa rekodi CAF

Gamondi Mshz Gamondi ataka Yanga kufuzu kwa rekodi CAF

Tue, 20 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 Jumamosi iliyopita dhidi ya Vital'O ya Burundi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema wanahitaji ushindi mwingine mkubwa katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, Jumamosi ijayo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Gamondi, alisema katika mchezo huo hawataenda kuzuia, au kulinda ushindi walioupata Jumamosi iliyopita, bali wanahitaji ushindi kwa mara nyingine tena na anadhani utakuwa mkubwa zaidi, kwa kuwa wanakwenda kucheza katika uwanja ambao watakuwa huru zaidi na mpira.

"Tunataka kushinda tena kwenye mchezo wa marudiano, wala hatuendi kuzuia, au kulinda ushindi wetu uliopita. Jumamosi ijayo tunacheza kama tulivyocheza mechi iliyopita, tunataka kufuzu, lakini tunataka kufuzu kwa kishindo," alitamba Gamondi, raia wa Argentina.

Alisema anamaanisha anachokiongea kwa sababu ana wachezaji bora wenye uwezo wa kuifanya kazi hiyo, ana kikosi kipana kwa sasa ambacho mchezaji anayeingia anakwenda kufanya kama kile kilichofanywa na aliyetoka au zaidi.

Gamondi alisema ana uhakika wa ushindi mkubwa zaidi kutokana na kwenda kucheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao ni mkubwa zaidi ya ule wa Azam Complex, utakaowafanya wachezaji wake wawe huru zaidi kutokana na aina ya mpira wanaocheza.

"Najua tunakwenda kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, tutacheza vizuri zaidi tofauti na ilivyokuwa Azam Complex, kwa sababu ni mkubwa zaidi na kutakuwa huru zaidi kwa aina yetu ya uchezaji mifumo yetu pia, ndiyo maana nasema tunaweza kupata ushindi mkubwa zaidi na kucheza soka safi zaidi ya mchezo uliopita.

Vital'O, iliutumia Uwanja wa Azam Complex hapa nchini, kama uwanja wao wa nyumbani, kutokana na kutokuwa na viwanja vilivyopitishwa katika michezo ya kimataifa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Gamondi pia alielezea hali ya hewa ilivyochangia wachezaji wake kutopata mabao mengi zaidi katika mchezo uliopita.

"Katika mechi iliyopita tuliathiriwa zaidi upepo, wachezaji wangu walinilalamikia kuhusu hilo, kwa hiyo walishindwa kufanya kwa usahihi baadhi ya mambo ikiwamo kupiga pasi sahihi, nadhani hilo pia lilichangia kupata idadi hiyo ya mabao, na inawezekana yangekuwa mengi zaidi kama isingekuwa hivyo, Jumamosi Uwanja wa Mkapa, mambo yatakuwa tofauti, mashabiki wa Yanga watafurahi zaidi," alisema.

Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Prince Dube, Clatous Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz Ki.

Wakati Gamondi akinena hayo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amewataka wanachama na mashabiki wa Yanga kumiminika kwa wingi Jumamosi ijayo, saa 1:00 usiku katika mechi hiyo ya mkondo wa pili huku akitangaza vingingilio vya mechi hiyo kuwa ni Sh. 30,000 kwa VIP A, Sh. 20,000 VIP B, Sh. 10,000 VIP C na Sh. 5000 kwa viti vya mzunguko 5000.

Alisema ushindi mnono walioupata Jumamosi iliyopita, utawafanya mashabiki wa timu hiyo kwenda uwanjani kama mtoko wa kifamilia, kwani hawatokaa kwa wasiwasi, badala yake watakuwa wanafurahia soka.

"Hatutakaa uwanjani kwa presha, mashabiki watakuwa wakiangalia mpira huku wakila na kunywa kwa furaha, huku wakifurahia soka, kwa hiyo sidhani kama ni mechi ya kukosa," alisema Kamwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live