Kocha Mkuu wa Yanga Sc, Miguel Gamondi amepinga utaratibu wa uongozi wa Klabu ya Yanga kuzipa majina ya wachezaji wao, mechi zao za nyumbani za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gamondi amesema hayo leo, Desemba 1, 2023 wakati akizungumza na wanahabri kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Al Ahly ambao Yanga wameupa jina la mchezaji wao beki wa kati, Ibrahim Hamad Bacca yaani Bacca Day.
Ikumbukwe kuwa, michezo miwili iliyopita ya michuano hiyo mmoja ambao Yanga walicheza na ASAS FC ya Djibouti waliupa jina la Maxi Day na mwingine shidi ya Al-Merrikh wakaupa jina la Aziz Ki Day.
"Sikubaliani kabisa na huu utaratibu wa kuita mchezo Jina la mchezaji kwa sababu mchezaji hayupo pekeake wapo timu, jambo muhimu kwangu ni timu sio mchezaji mmoja binafsi.
"Ila naelewa ndio utaratibu wa timu kwa ajili ya kufanya marketing, kuwafanya mashabiki waje uwanjani na kuuelewa zaidi mchezo husika najua huo ndio utaratibu wa klabu kuhamasisha ila sio utaratibu mzuri kwangu mimi binafsi," amesema Kocha Gamondi.