Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi apigiwa simu ya tahadhari

Miguel Gamondi Maboa Kesho Gamondi apigiwa simu ya tahadhari

Tue, 13 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Haloo Gamondi. Nakupigia simu hii ni ya muhimu sana. Tafadhali usiache kuipokea. Nataka nikukumbushe kuwa muda wa mapumziko ya kupisha Kombe la Mapinduzi na Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) umepita.

Nakupigia kocha Gamondi kukwambia kwamba haya matokeo ambayo Yanga inapata kwa taabu 0-0 dhidi ya Kagera Sugar, 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, 2-1 vs Mashujaa au 2-1 Tanzania Prisons, sio matokeo ya Yanga tuliyoizoea katika siku za hivi karibuni.

Yanga tuliyoizoea inawapiga watu bao 5 na  mpira unapigwa mwingi sana. Kocha Gamondi nimekupigia kukumbusha kwamba zimebaki siku 10 tu wanakuja wale Belouizdad kwa ajili ya mechi yenu ya Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika Februari 24 Kwa Mkapa. Ndio Belouizdad, walewale ambao waliitia doa Yanga kule kwao Algeria kwa kuichakaza 3-0.

Ndio tunakumbuka kwamba kule Yanga ilicheza soka safi, magoli wakafunga Waarabu, lakini tunapenda kukumbusha kwamba kwa mwendo wa sasa, Yanga ikizubaa hivi itajikuta inapigiwa boli jingi na kufungwa magoli pia.

Kwani si unaona jinsi ambavyo Yanga inaruhusu mabao katika siku za karibuni? Katika michezo mitano iliyopita ya Ligi Kuu ya Algeria, Belouizdad imeruhusu mabao matatu huku yenyewe ikifunga mabao manane yaani imeshinda mechi tatu (3-1 vs JS Saoura, 2-0 vs MC Oran na 2-0 dhidi ya timu inayoshika mkia ya US Souf juzi Jumamosi), pia imepata kipigo kimoja cha mabao 2-1 kutoka kwa El Bayadh inayoshika nafasi ya 11 katika ligi hiyo ya timu 16 na imetoka suluhu moja (0-0 vs Biskra inayoshika nafasi ya 8 katika msimamo).

Kocha Gamondi najua unafahamu lakini nakukumbusha tu, Belouizdad ambayo katika kundi D inashika nafasi ya tatu ikiwa na  pointi 4, yaani moja nyuma ya Yanga iliyo nafasi ya pili kwa pointi 5, itacheza Ijumaa hii Februari 16 mechi yake ya kiporo nyumbani dhidi ya Al Ahly. Ikilazimisha japo sare itaishusha Yanga hadi nafasi ya tatu katika msimamo kwan ikifikisha pointi 5 tu kama za Yanga itakaa juu ya Wananchi kwa sababu ina tofauti nzuri ya mabao ya kufunga +2 wakati Yanga ina GD 0.

Kwa maana hiyo, Belouizdad ikipata sare tu nyumbani Ijumaa, itakuja Dar ikiwa katika nafasi ya pili katika msimamo na mechi itakuwa ngumu zaidi. Katika mechi ya Dar Yanga ni lazima icheze kiwerevu zaidi ya ilivyocheza kule Algeria ilikolala 3-0.

Ili kucheza hivyo ni lazima kutambua vitu muhimu. Kwanza kwamba katika hizi mechi za kimkakati matokeo ya mechi zilizopita au za kwenye ligi sio muhimu sana.

Ndio maana Marumo Gallants ya Afrika Kusini ilifika hadi nusu fainali ya Kombe la Shirikisho kabla ya kutolewa na Yanga msimu uliopita, wakati katika ligi ya kwao ilishuka daraja.

Kwa mantiki hiyo, mechi hizi za CAF ni za kimkakati sio za kuangalia ulipata matokeo gani jana.

Hivyo nakukumbusha Gamondi uliweke sawa jeshi lako. Maana huku CAF kunaweza kukuhukumu. Mafanikio ya mtangulizi wako Nasreddine Nabi yanaweza kutumika kama fimbo ya kukuchapia ukizubaa.

Yanga baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita inaamini inastahili kufika angalau robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kutokana na kikosi kilichoboreshwa.

Yanga hii kwa kuwapata Pacome Zouzoua, Yao Kouassi na Maxi Nzengeli imeongezeka ubora kwa sababu mabao yanatoka pande zote za uwanja.

Pengo pekee ambalo halijazibika ni la straika Fiston Mayele. Alikuja Hafiz Konkoni viatu vilimzidi ukubwa. Na sasa yupo Joseph Guede, ambaye pengine ana kitu lakini anahitaji muda kwa sababu kwa sasa uwanjani anaonekana kuifanya Yanga kucheza na watu 10 kwa muda mwingi kwa sababu haonekani kuhusika na  mchezo kwa muda mwingi.

Augustine Okrah alishindwa kung'aa Simba, watu bado wana maswali mengi kama ataweza kung'aa Yanga. Hili ni la kusubiri na kuona, simu yangu inataka kukata, ngoja nimalizie haraka.

Shekhan Ibrahim ni kijana anayeinukia vyema, baada ya kusajiliwa katika dirisha dogo anapaswa kupewa muda kidogo kidogo kwa sababu anaonyesha matumaini makubwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi mpenyezo na  mashuti ya mbali. Yale mashuti yake kocha Gamondi utayahitaji sana utakapokutana na timu zinazopaki basi.

Kocha Gamondi nakukumbusha kuwa hizi sio mechi za majaribio. Kuwapa nafasi watu ni muhimu lakini kumbuka dakika ni 90 tu, hivyo ni muhimu kuutumia muda vizuri muda huu, kama Guede ameshindwa kufunga  ndani ya dakika kadhaa, usilazimishe kusubiri muujiza.

Waamini ambao wameshafanya kitu angalau kwenye mechi za kawaida badala la kutarajia makubwa kwa ambaye anajitafuta. Lakini simaanishi usimpe nafasi. Lakini anza na mziki kamili halafu wengine waje kuchangia mechi ikiendelea.

Kiungo hakina shida sana. Kuna mafundi wa kutosha. Khalid Aucho ni masta pale. Mudathir Yahya ni chanzo kingine muhimu cha mabao kwa sababu ameshathibitisha anafunga mara kwa mara.

Salum Aboubakar 'Babu Kaju' anakupa chaguo pana zaidi pale kati maana akicheza mara nyingi hutawala dimba lote. Zawadi Mauya yuko sawa. Jonas Mkude ni mzoefu wa hizi kazi atakusaidia akihitajika.

Ila Gamondi nikukumbushe kitu. Nahodha wako Bakary Mwamnyeto anachomesha sana siku hizi. Anajua boli na anajua kuanzisha mashambulizi, tatizo kama anajisahau ama anajiamini sana, matokeo yake anachoma nyumba sana au wenzake kina Ibrahim Bacca na  Dickson Job mara kwa mara wanalazimika kuja kuokoa jahazi. Mwambie atulize akili uwanjani na  asiwe mzito kuamua jambo.

 Hata wewe pia Gamondi usizubae sana kufanya mabadiliko kama timu haitembei badili mtu au watu haraka kwa sababu dakika ni 90 tu.

Halafu pia... hallow hallow. Gamondi, Gamondiii... naona simu imekata, daah! yangu kumbe ndiyo imeisha chaji, sijui umeme utarudi saa ngapi!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live