Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi apiga mahesabu makali Makundi CAFCL

Gamondi X CBE Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.

Thu, 19 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

HUKU bado wakiwa hawajatinga hatua ya makundi wakisubiri mchezo wa marudiano hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, ameanza kupigia hesabu hatua ya makundi, akiweka wazi ili kufika hatua ya robo fainali au zaidi itategemea zaidi kundi watakalopangwa.

Gamondi amesema kuna wakati inatokea wanapangiwa timu ngumu na kuwa na kazi kubwa ya kusonga mbele.

Gamondi alisema hawezi kusema wanataka kufika wapi kwenye Ligi ya Mabingwa, badala yake sasa hivi wanaangalia makundi tu mpaka pale yatakapopangwa makundi ndipo watakapojua hilo kutokana na aina ya timu ambazo watakutana nazo.

"Yanga ni klabu ambayo kila msimu inatakiwa iwe kileleni, hivyo kufuzu makundi ni jambo ambalo linaweza kutokea na tuna matumaini sana.

"Baada ya hapo huko mbele tutaona nini kitatokea kwani ni bahati pia kwa upangaji wa makundi, unaweza kupata kundi rahisi au gumu. Mfano kundi letu msimu uliopita lilikuwa gumu, kulikuwa na CR Beloizdad ya Algeria, Al Ahly ya Misri, hatua ya robo fainali tukakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, kwa maana hiyo kujua utafika wapi inategemea na njia unayopitia," alisema Gamondi.

Kauri hiyo ya Gamondi inaweka wazi matumaini yake makubwa ya timu yake kutinga hatua ya makundi kwenye mchezo wao wa Jumamosi utakaochezwa 2:30 usiku dhidi ya CBE ya Ethiopia, Uwanja wa New Amaan Zanzibar.

Hiyo inachagizwa na mchezo wa kwanza uliochezwa Jumamosi iliyopita, Uwanja wa Abebe Bikila, Addis Ababa, Ethiopia, Yanga ilipopata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji raia wa Zimbabwe, Prince Dube.

Wakati hayo yakiendelea, Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison, ameeleza ni kwa nini mchezo huo wa marudiano umepelekwa Zanzibar badala ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ilivyo kawaida.

Alisema baada ya kufanya tathmini wamegundua kuwa Zanzibar kuna mashabiki wengi wa Yanga ambao nao wanahitaji kushuhudia michezo hiyo ya kimataifa.

"Tumeshacheza sana kwenye uwanja huu, kama utakumbuka mechi yetu ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam tulipata ushindi, Zanzibar ni sehemu ya Tanzania na tuna mashabiki wengi sana hakuna mtu mwenye shaka na hilo, tulifanya tathmini ya kina na tukaona ni sehemu sahihi ya kwenda kucheza mchezo wetu wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Mungu akijaalia tutaingia kwenye hatua ya makundi," alisema meneja huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live