Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi apewa panga kufyeka Yanga

Gamondi Miguel Tizi Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, amesema mchezaji yeyote wa timu hiyo ambaye hakuonesha kiwango katika michuano ya Kombe la Mapinduzi hafai kuichezea timu hiyo.

Rais huyo amempa rungu Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, kuwaacha wachezaji ambao anaona hawawezi kumsaidia katika kutimiza malengo yake na ya klabu katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Hersi amesema Yanga ni klabu kubwa, hivyo haiwezi kukaa na mchezaji ambaye hawezi kuisaidia timu hiyo hata kwenye michuano ya muda mfupi tu kama Kombe la Mapinduzi.

"Nawapongeza waandaaji wa michunao ya Kombe la Mapinduzi, na vijana wetu chini ya miaka 20 ambao wameshiriki Kombe la Mapinduzi, wameonyesha thamani ya kuvaa jezi ya Yanga.

"Ila kama kuna mchezaji ambaye hakuonesha kiwango chake katika michuano kama hiyo na kutupa ushindi, sisi Wanayanga tuliomtuma huyo mchezaji kwetu hawezi kuwa na nafasi tena, wapi sasa atatupa matokeo mazuri na kuonesha kiwango chake?

"Mchezaji ambaye hajaweza kutimiza majukumu yake kwenye uwanja, huyo hafai kuwa na klabu yetu, kocha tumempa mamlaka ya kumwondoa yeyote ambaye anaona hatufai," alisema rais huyo.

Yanga imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa mabao 3-1 na APR ya Rwanda Jumapili iliyopita.

Baada ya kutolewa, Kocha Mkuu Gambondi alisema mbali na kuwatumia vijana chini ya miaka 20, lakini alitumia baadhi ya wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kwenye mechi nyingi za Ligi Kuu, achilia mbali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Injinia Hersi pia amepinga madai kuwa ana wachezaji wake anaowapenda zaidi kuliko wengine, akisema amehusika na usajili wa wachezaji wote kwenye klabu hiyo.

"Katika wachezaji hawa wa Yanga ninahusika kwa asilimia 99 mpaka 100 kuwasajili, hivyo siwezi kuwabagua wengine na kuwapendelea baadhi.

"Wote nimewasijili mwenyewe, ni mchezaji mmoja tu ambaye sijahusika kwenye usajili wake naye ni Metacha Mnata kwa sababu wakati naingia Yanga nilimkuta, lakini aliondoka na baadaye akarejea tena Yanga na safari hii mimi nikahusika, wote wamepita mezani kwangu, hivyo hakuna mchezaji ambaye kwangu ana thamani kuliko mwingine.

"Mchezaji yeyote anayecheza timu hii ya Yanga ni mchezaji wangu, ninathamini wachezaji wote waliopo hapa bila kujali amesajiliwa na nani," alisema Hersi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live