Mchezo wa kwanza wa Yanga kwenye ushindani ndani ya msimu wa 2023/24 ni dhidi ya Azam FC, huu utakuwa mchezo wa ufunguzi katika hatua ya Ngao ya Jamii ikiwa ni mfumo mpya utatumika.
Ni mwendo kama wa ligi na timu nne zitashiriki zile zilizogotea nafasi nne za juu ikiwa ni Yanga ambao ni namba moja, Simba namba mbili. Azam FC namba tatu huku Singida Big Stars kwa sasa ni Singida Fountain Gate iligotea nafasi ya nne.
Yanga inatarajiwa kumenyana na Azam FC, Uwanja wa Mkwakwani Tanga Agosti 9 2023 na ikumbukwe kwamba ni wao walitwaa Ngao ya Jamii msimu wa 2022/23 kwa kuwatungua Simba mabao 2-1.
Miongoni mwa nyota ambao wameanza mazoezi na Yanga iliyoweka kambini Avic Town Kigamboni kwa Yanga ni Mudhathir Yahya, Khalid Aucho, Jonas Mkude.
Yanga ipo chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi ambaye amerithi mikoba ya Nasreddine Nabi raia wa Tunisia.
Swali la kwanza ambalo Yanga watamuuliza Gamondi ni je, atatwaa ushindi wa Ngao ya Jamii kama alivyofanya kocha Nabi kwa misimu miwili mfuflulizo?
Majibu anayo kocha gamondi, benchi lake la ufundi, wachezaji wake, lakini kwa mashabiki, matarajio yao makubwa ni kuona yanga inafanya zaidi ya kile ilichokifanya msimu uliopita, hivyo hesabu zao za kwanza ni kuhakikisha wanachukua Ngao ya Jamii kisha wapige hesabu za Ligi na michuano mingine.
Tayari Yanga imeshakamilisha usajili wa wachezaji wake saba ambapo wa kigeni ni watano na wazawa ni wawili pekee na sasa wamejichimbia Avic Town kujifua kabla ya kuanza msimu.
Gamondi, kocha mwenye wasifu mkubwa, ni muumini wa soka la kumiliki mpira na kushambulia kwa kasi, ndiyo maana utaona ameongeza viungo wa kati pamoja na mabeki na washambuliaji wa pembeni wenye kasi kama Maxi Nzengeli na Skudu Makudubela.
Je, Gamondi atafanikiwa kufanya makubwa zaidi ya Nabi?