Klabu ya Yanga imerejea mazoezini Avic Town, Kigamboni ikijiandaa na mechi zijazo ikiwemo ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar itakayopigwa Disemba 16.
Lakini kwenye timu hiyo ni wazi mawinga (viungo wa pembeni) halisi wa timu hiyo kazi wanayo msimu huu chini ya kocha Miguel Gamondi kwani ameonekana hana kipaumbele kwenye upande huo.
Tangu kutua Yanga na kuanza kazi rasmi mwanzoni mwa msimu huu, Gamondi ameonekana kuwa muumini sana wa viungo kuliko mawinga jambo linalowapa tabu mawinga wa timu hiyo kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho na muda mwingi kusota benchi.
Mawinga asilia ndani ya Yanga ni watano, Jesus Moloko, Farid Mussa, Denis Nkane, Mahlatse Makudubela 'Skudu', na Maxi Nzengeli ambaye amebadilishiwa majukumu na kuwa kiungo mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji.
Gamondi ni muumini wa mfumo wa 4-2-3-1, ambao mara nyingi umekuwa ukihusisha viungo watano na wakati mwingine ametumia mifumo ya 5-1-2-2, na 3-5-2, ambayo yote huwa na viungo wengi wa kati uwanjani.
Hali hiyo imemfanya Gamondi kumbadilishia majukumu yake halisi Maxi, na kumtumia kama kiungo mshambuliaji akicheza maeneo sawa na Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki ambao huwa wanabadilika wakiwa uwanjani wakati mpira ukichezwa.
Maxi amecheza mechi zote za Yanga kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu akitumika kwa dakika 1284.
Winga wa zamani Yanga, Saidi Maulid 'SMG' alisema ni jukumu la mawinga waliopo kwenye timu hiyo kupambana na kuhakikisha wanamshawishi kocha awapange.
"Kila kocha anataka kutumia wachezaji walio tayari, nadhani anaowapanga kwa sasa anaona ndio watamfaa hivyo mawinga wa Yanga waongeze juhudi na wakifanya vizuri mazoezini sidhani kama ataacha kuwapa nafasi kwenye mechi," alisema SMG.
Mifumo na falsafa hizo za Gamondi imekuwa dozi chungu kwa mawinga Moloko, Nkane, Skudu na Farid ambao msimu uliopita walikuwa wakicheza mara kwa mara lakini sasa ni nadra sana kuwaona.
Katika takwimu ilizonazo Mwananchi, Yanga imecheza jumla ya mechi 16, za Ligi Kuu (9) na Ligi ya Mabingwa Afrika (7) ikiwa ni sawa na dakika 1620 lakini Skudu, Moloko, Nkane na Farid hakuna hata mmoja aliyecheza walau robo ya dakika hizo kwani Moloko ndiye amecheza nyingi kati yao akidumu uwanjani kwa dakika 323 tu.
Katika mechi tisa za ligi ilizocheza Yanga Moloko amecheza nne tu, akianza kikosini katika mechi ya kwanza dhidi ya KMC na kutolewa dakika ya 79, mchezo uliofuata dhidi ya JKT hakucheza baada ya hapo dhidi ya Namungo aliingia akitokea benchi na kucheza kwa dakika 23, ikafuata mechi na Ihefu aliyocheza dakika 68 tu huku akikosa nne mfululizo dhidi ya Geita, Azam, Singida na Simba na kuibukia kwa Coastal alipocheza kwa dakika 21 tu huku akiwa na pasi za mabao mbili.
Mechi za kimataifa kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imecheza saba ikianza na Asas ugenini ambapo Moloko hakucheza lakini ile ya marudiano alicheza dakika 46, zikafuata mechi mbili na El Merrikh ya Sudan ambapo mchezo wa kwanza alicheza dakika moja tu na marudio akacheza dakika 76.
Nyota huyu ambaye alikuwa na uhakika kwenye kikosi cha Yanga msimu uliopita, msimu huu kwenye hatua ya makundi hadi sasa amecheza mechi moja tu dhidi ya CR Belouizdad akicheza kwa dakika tisa pekee.
Upande wa Farid Mussa ambaye msimu uliopita alikuwa na uhakika wa kucheza, mbele ya Gamondi mambo yamembadilikia kwani kwenye ligi hadi sasa amecheza mechi moja tu dhidi ya KMC alipoingia dakika 26 za mwisho huku kwenye zile saba za kimataifa akiwa hajacheza hata dakika moja licha ya kumudu pia kucheza kama beki wa kushoto .
Nkane ni kama vile hayupo kwenye mipango ya Gamondi kwani kwenye ligi hadi sasa amecheza michezo mitatu kati ya tisa ya Yanga. Aliingia dakika za jioni dhidi ya KMC dakika 11 za mwisho, ikafuata na JKT akacheza dakika 12 tu kisha ile na Geita Gold aliyocheza dakika 17 tu huku kwenye zile mechi saba za kimataifa akiambulia dakika 44 tu katika mechi ya marudiano dhidi ya Asas.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema kila kocha ana falsafa zake na kinachofanyika sasa ni maamuzi ya Gamondi.
Mwaisabula alisema Nabi (Nasreddine) alikuwa ni muumini wa kuchezesha wachezaji wengi kwa maana ya kumpa nafasi kila mchezaji kuitumikia timu jambo ambalo lilikuwa faida kwa wachezaji wenyewe, Yanga na hata Taifa kwani wazawa wengi walipata muda wa kucheza.
"Kwa Gamondi mambo yamebadilika, ana watu wake wachache anaowaamini na mechi nyingi wanacheza wale wale na mfumo ni mmoja ambao hauwapi nafasi mawinga kwani anatumia zaidi viungo;
"Hii sio kwa mawinga tu kuna hata viungo waliopoteza nafasi kama Salumu Abubakar 'Sure Boy', ambaye kwa Nabi alikuwa mchezaji tegemeo, kiufupi yote hayo ni maamuzi ya Gamondi lakini binafsi sioni kama yana afya kwa timu katika siku zijazo."
Wakati huo huo upande wa Skudu aliyesajiliwa Yanga msimu huu akitokea Marumo Gallants ya Afrika Kusini, mambo yamekuwa magumu katika kikosi cha Gamondi kwani hadi sasa amecheza mechi tatu tu kati ya tisa ilizocheza Yanga kwenye ligi akianza dhidi ya Ihefu na kucheza kwa dakika 57, akacheza dakika 18 mbele ya Singida Bs na dakika moja tu dhidi ya Simba.
Kimataifa Skudu amecheza dakika 14 tu kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Al Merrikh.
Kwenye mahojiano na Wanahabari baada ya mechi iliyopita kimataifa dhidi ya Medeama kumalizika, Gamondi aliulizwa swali kuhusu mabadiliko ya wachezaji kikosini na kujibu kwa ufupi tu; "Ni maamuzi yangu."
Mechi ijayo ya Yanga itacheza Desemba 16 uwanja wa Azam Complex dhidi ya Mtibwa Sugar iliyo nafasi ya mwisho kwenye ligi ikiwa na alama tano baada ya kucheza mechi 12, huku Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi 24 ilizovuna kwenye mechi tisa.