Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi ana siku 38 Yanga

Gamondiz1462 Gamondi ana siku 38 Yanga

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi na mastaa wa timu hiyo wasiokuwepo kwenye fainali za Afcon 2023, wana siku 38 za kibabe za kujiweka tayari kabla ya kurejea kwenye michuano mbalimbali ikiwamo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga itakuwa kambini kwa siku hizo kabla ya kuanza kucheza mechi za michuano hiyo itakayorejea tena mara baada ya Afcon 2023 inayoendelea Ivory Coast, ambapo Tanzania inashiriki kwa mara ya tatu na itaanza kibarua keshokutwa dhidi ya Morocco katika mechi ya Kundi F.

Gamondi anakabiliwa na mechi mbili za kumalizia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazochezwa kati ya Februari 23 na Machi 1, lakini ina Ligi Kuu Bara itakayorudi mapema mwezi ujao kama ilivyo kwa kiporo cha ASFC dhidi ya Hausing ya Njombe.

Akizungumza mapema juzi, kocha huyo alisema ametaka wachezaji wote kuanza kambi rasmi leo ili kurekebisha yaliyojitokeza kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na timu hiyo ilitolewa robo fainali kwa kufungwa mabao 3-1 na APR ya Rwanda.

Gamondi alisema muda alionao kwa sasa wa kuwalisha madini wachezaji wa timu hiyo kabla ya kuja kuungana na wenzao waliopo fainali za Afcon anaamini atapata fursa ya kurekebisha kila dosari na kuwaimarisha wachezaji waliokuwa majeruhi na wale waliochemsha katika Mapinduzi.

Katika michuano hiyo iliyomalizika juzi kwa Mlandege kubeba tena ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo, ikiifunga Simba kwa bao 1-0, Gamondi aliwatumia wachezaji vijana na wale wasio na namba katika kikosi cha kwanza, huku akiwapa mapumziko baadhi ya mastaa akiwamo Pacome Zouzoua, Yao Kouassi, Khalid Aucho na wengine.

“Huu ni muda wa kurekebisha mambo, kwani bado tuna kazi kubwa mbele yetu. Tunaamini hadi wale waliopo fainali za Afcon, kila kitu kitakuwa sawa. Tumeona kila kitu kupitia Mapinduzi na sasa ni muda wa kutengeneza mipango ya mechi zijazo,” alisema Gamondi.

Yanga iliyopiga kambi Avic Town, Kigamboni katika Ligi ya CAF, itaanza kucheza na CR Belouizdad ya Algeria Februari 23 ikiwa na kazi ya kulipa kisasi cha 3-0 ilichopewa ugenini katika mechi ya kwanza, kisha kuifuata Al Ahly ya Misri inayoongoza Kundi D jijini Cairo Machi 1.

Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi tano, nyuma ya Al Ahly yenye pointi kama hizo ila ikibebwa na uwiano wa mabao yenye mchezo mmoja mkononi dhidi ya CR Belouizdad.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: