Kocha Mkuu wa Young Africans, Muargentina, Miguel Gamondi anasuka kikosi chake kwa ajili ya mechi zijazo ikiwemo ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merrikh ya Sudan.
Mchezo huo utakaopigwa Septemba 16 mwaka huu, jijini Kigali huku akijiandaa kuwasapraizi wapinzani hao kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Timu hizo zitakutana kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kurudiana majuma mawili baadae na mshindi wa jumla kutinga makundi, huku kocha Gamondi akifahamu Wasudani wameshampiga chabo amepanga kwenda kuwasapraizi ugenini akipanga kumtumia winga Msauzi, Mahlatsi Makudubela Skudu aliyerejea uwanjani tangu alipoumia mwezi uliopita kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC.
“Kila mchezaji wa Young Africans ana nafasi kikosini hivyo napenda kuwaona wote wakiwa timamu kwani wanatupa matumaini na wigo mpana wa kupanga kikosi kwenye mechi.” Amesema Gamondi
Skudu alijiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akitokea Marumo Gallants ya Afrika Kusini, tangu atue amecheza mechi mbili tu, ya Wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs na ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC aliyoumia dakika ya saba na kushindwa kuendelea na mchezo huo.
Baada ya hapo Young Africans ilicheza mechi tano za kimashindano bila Skudu, moja ikiwa ni fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC, mbili za Ligi Kuu na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali jambo linalowafanya mashabiki wa Young Africans kuwa na shauku ya kumuona mkali huyo wa chenga na kuchezea mpira.
Baada ya mechi ya kirafiki, Young Africans itaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya Septemba 14 kusafiri hadi Kigali, Rwanda kwa mchezo wa kwanza na Al Merrikh katika mchezo wa kwanza kabla ya marudiano utakaopigwa Septemba 29.