Huwezi tenganisha dhambi ya kudanganya umri na wachezaji wanaopatikana magharibi mwa Africa. Hati ya kusafiria inaonyesha ana miaka 26.
Akiwa amezaliwa April 30th 1997. Ufanisi bora akiwa kazini. Ni kitu ambacho kinaua mjadala wa umri wake.
Begi mkononi, blichi kichwani kama sehemu ya kumuenzi marehemu Ndanda Cosovo. Hivi ndivyo alivyotua airport ya mwalimu Nyerere. Akiwa mchezaji mwenye CV ya kawaida.
Isiyoweza kumshawishi hata Christian Bella amrushe kwenye ngoma zake.
Taratibu akaanza mchakato wa kujitwalia utukufu. Uhodari wa ku drible, kuwafuata mabeki kwa kasi, kisha kuzipelekea moto wa mauti nyavu. Huu ni wino alioutumia kuwalazimisha mashabiki wa Yanga. Waliandike jina lake kwenye kuta za mioyo yao.
Kama mashabiki wa Yanga wakipewa tenda ya kuandika biblia ya soka leo. Naamini jina la 'Peodoh Pacome Zouzoua' wataliweka sehemu ya injili.
Hatuhitaji elimu ya unajimu kukubali kuwa, Pacome ni namba 10 mwenye uwezo wa kucheza timu yoyote barani Africa. Alikuja Tanzania akiwa hana ukubwa alionao sasa. Anachokifanya kila siku, ni kuitumia Yanga kama jukwaa la kunadi bidhaa za miguu yake.
Elimu ya darasa la 7 inatosha sisi wote kukubaliana hili. Bila uwepo wa 'Pacome' Yanga ingekuwa bado inahangaika kuonja radha ya ushindi wa mechi za hatua ya makundi, CAF champions league.
Katika safari ya kuutafuta ukubwa ndani ya bara la Africa. "Gamondi" amemgeuza "Pacome" silaha ya sumu. Pacome ndiye master plan wa kila vita kwenye mechi za kimataifa. Gamondi amemkabidhi Pacome funguo zote za milango ya uovu.
Pacome ni material iliyotengenezwa Asec mimosas. Pale ni chuo kikuu cha soka la Ivory coast. Asec huwa wana deal na watu wenye miguu ya dhahabu tu. Wakishaipitisha kwenye chungu cha moto wanaiweka sokoni. Asec huwa hawazalishi bidhaa chafu.
Yanga walipofanikiwa kuipata sahihi ya mkono wa Pacome. Yalikuwa matumizi sahihi ya pesa pamoja na rasilimali muda.