Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi amaliza sherehe Yanga

Pacome Gamondi Maxi Gamondi amaliza sherehe Yanga

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga baada ya kumalizana na Mnyama siku tatu zilizopita watakuwa jijini Tanga leo, Jumatano kucheza dhidi ya wenyeji, Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani, huku kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akiwaambia mastaa wake, “sherehe imemalizika.”

Wakati Yanga yenye pointi 21 ikihitaji kuendelea kujikita kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Bara, Coastal inahitaji kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja kufuatia kuwa na mwenendo mbaya ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi wenye timu 16 na pointi saba sawa na Tanzania Prisons na Geita Gold ambazo zipo chini.

Vijana wa Gamondi watashuka dimbani huku wakiwa na morali kubwa kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Simba Jumapili iliyopita, lakini Coastal licha ya kuwa nyumbani itakuwa na wakati mgumu kwani katika michezo mitano iliyopita imeshinda mmoja dhidi ya Mashujaa, Oktoba 25 huku ikipoteza dhidi ya Azam FC (1-0) na suluhu dhidi ya Namungo, Ihefu na Tabora United.

Hii itakuwa ni vita kati ya timu iliyopo kwenye kiwango bora zaidi kwa sasa, Yanga ambayo imeshinda mechi nne mfululizo tangu ilipopoteza mara ya mwisho, Oktoba 4 dhidi ya Ihefu kwa mabao 2-1.

Dhidi ya Coastal ambao kwa kuzingatia ubora kwa sasa ‘fomu ya timu na siyo msimamo’ inashika nafasi ya 10 huku Yanga ikiwa ya kwanza kwenye msimamo, hiyo inatoa picha kuwa kocha wa Wagosi wa Kaya, Fikiri Elias ambaye kikosi chake kimefunga mabao manne huku kikiruhusu mabao saba atakuwa na wakati mgumu kwenye mchezo huo.

Yanga imefunga mabao 25 kwenye michezo minane iliyocheza huku ikiruhusu matano na vinara hao wenye safu kali zaidi ya kiungo wana wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi.

MKWAKWANI PAGUMU

Rekodi zinaonyesha miongoni mwa viwanja vigumu kwa Yanga ni pamoja na CCM Mkwakwani kwani katika michezo sita ya mwisho dhidi ya Wagosi hao, imeshinda mara mbili, kupoteza mara mbili huku ikitoka sare mara mbili. Licha ya ugumu huo ndani ya misimu miwili iliyopita Yanga imeshinda mfululizo kwa mabao 2-0 kwenye kila mchezo na aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Fiston Mayele akifunga bao moja kwenye kila mchezo.

Yanga bila Mayele na Bernard Morrison ambao walifunga kwa mara ya mwisho Mkwakwani, inarejea tena kwenye uwanja huo ikiwa na maingizo mapya kama vile Yao Kouassi ambaye ni beki wa kulia lakini anaongoza kwa asisti akiwa nazo tano Ligi Kuu Bara, Maxi Nzengeli mabao saba na Pacome Zouzoua manne, huku supastaa Aziz Ki akiwa na saba.

Misimu ambayo Mkwakwani kumekuwa kugumu kwa Yanga ni 2020/21 ambapo ilifungwa mabao 2-1, 2019/20 suluhu, 2018/19 sare ya bao 1-1 na 2016 ikapoteza 2-0.

MSIKIE GAMONDI?

Kocha wa Yanga, Gamondi amewaeleza wachezaji wake kuwa sherehe ya kuwafunga watani zao imeisha na sasa ni kuelekeza nguvu kwenye mchezo huo kama ilivyokuwa dhidi ya Simba ili kuhakikisha wanaendelea kukusanya pointi tatu kwenye kila mchezo ambao utakuwa mbele yao.

“Nina furaha sana kuwa na kundi hili la wachezaji. Kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akijitoa kuhakikisha alichonacho kinakuwa na manufaa kwa ajili ya timu. Coastal ni timu nzuri, hivyo tunatakiwa kuendelea kujitoa na kupigania pointi,” alisema kocha huyo.

“Haijalishi utofauti wetu wa pointi ukoje jambo muhimu kwetu ni kuendelea kukimbia bila ya kuangalia nyuma yetu nani anatufuata. Tutaupa uzito mchezo mmoja baada ya mwingine.”

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Gamondi kuongoza kikosi chake kwenye uwanja huo kwani mwanzoni mwa msimu alifanya hivyo katika michezo miwili ya ufunguzi wa msimu ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na Simba.

COASTAL HAITISHWI

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Coastal Union FC, Fikiri amesema licha ya ubora ambao Yanga iliuonyesha kwenye mchezo dhidi ya Simba, lakini wao wanaamini watatumia udhaifu ilionao kutafuta ushindi.

“Tunajua ubora wa Yanga ulipo, kwa hiyo tutacheza kwa kuwaheshimu huku tukitumia udhaifu wao ambao kama benchi la ufundi tumeuona ili kutafuta matokeo chanya. Tunawaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutupa sapoti,” alisema kocha huyo.

Coastal Union ambao mara ya mwisho walicheza Novemba Mosi dhidi ya Namungo na kuvuna pointi moja baada ya kutoka suluhu, walikuwa na siku saba za kujiandaa kukabiliana na mabingwa hao watetezi wa michuano ya Ligi Kuu Bara.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: