Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi alivyowapiga chenga ya mwili Mamelodi

Gamondi Yanga Ms Gamondi alivyowapiga chenga ya mwili Mamelodi

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi mjanja sana. Baada ya kugundua kwa vyovyote vile wapinzani wao katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ingetuma mashushushu wa kuifuatilia timu hiyo, jana usiku aliamua kuwapiga chenga wakati ikicheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Mamelodi katika mechi ya mkondo wa kwanza itakayochezwa siku ya Machi 30 kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kurudiana nao wiki moja baadae Afrika Kusini na mshindi atafuzu nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Jana usiku, Yanga ilikuwa ikicheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold na Gamondi aliamua kuwapanga wachezaji tofauti na wale wa kikosi cha kwanza, licha ya mashushushu wawili wa Mamalodi akiwamo Mchambuzi wa Video (Video Analyst), Dayle Solomon na Sibusiso Makitla (Performance Manager) ili kuja kuisoma Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Gamondi alichofanya kwenye mchezo huo ulioshuhudiwa Stephane Aziz KI akifunga bao la 13 msimu huu katika ligi hiyo, alipangua kwa kiasi kikubwa kikosi chake cha kwanza ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu kupumzika.

Miongoni mwa wachezaji ambao hawakuanza kwenye mchezo huo ni pamoja na Mudathir Yahya ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango bora, Pacome Zouzoua, Ibrahim Hamad 'Bacca' na Kouassi Attohoula Yao ambaye ilimbidi kuingia mwishoni kwa kipindi cha kwanza baada ya Kibwana Shomary kupata majeraha.

Hata hivyo, licha ya Gamondi kufanya mabadiliko hayo kwa kutoa nafasi kwa Kibwana, Augustine Okrah, Gift Fred na Dickson Job akicheza nafasi ya kiungo tofauti na ilivyozoeleka, Yanga ilionyesha kiwango kizuri kipindi cha kwanza na kupata bao pekee lililowapa ushindi katika mchezo huo.

Muda mwingi wa mchezo, watu hao wawili wa Mamelodi ambao walikaa jukwaa kuu walionekana kuandika huku wakisemezana, kwa mujibu wa taarifa inaelezwa wataendelea kuwepo nchini hadi Jumapili na Yanga itakuwa na mchezo mwingine mgumu wa ligi dhidi ya Azam FC kabla ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.

Ikumbukwe siku chache zilizopita kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena alisema ataanza kuifuatilia Yanga wakati wa michezo ya kimataifa, hivyo watu hao wapo hapa kwa ajili ya kudukua taarifa muhimu ambazo zitakuwa msaada kwa benchi la ufundi la timu hiyo wakati wakijiandaa na mchezo huo.

Kwa upande wa Gamondi amesema ilimbidi kufanya mabadiliko hayo kutokana na mechi mfululizo walizonazo hivyo alitunza nishati ya baadhi ya wachezaji wake ili kufanya vizuri wikiendi ijayo dhidi ya Azam ambao nao walikuwa wakiifuatilia Yanga kwenye mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wao.

"Tumekuwa na mechi nyingi mfululizo, nina furaha kwa matokeo ambayo tumeyapata, nadhani tulikuwa bora pamoja na uchovu ambao wachezaji wapo nao tumefanya kile ambacho kilitakiwa kufanyika, bado tuna mchezo mwingine mgumu mbele yetu kabla ya kuwa na mapumziko mafupi," amesema kocha huyo.

Mara baada ya kumalizana na Azam FC na kupita kwa wiki ya kalenda ya FIFA, Yanga itaanza maandalizi ya mchezo huo wa CAF ili kutaka kupata matokeo mzuri nyumbani kabla ya April 6 kurudiana huko Sauzi na kuandika rekodi ya kucheza nusu fainali kwa mara ya kwanza kwa klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live