Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi alimuiga Simeone akapata kitu, tukutane Pretoria

Gamondi X Mokwena Gamondi alimuiga Simeone akapata kitu, tukutane Pretoria

Tue, 2 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Mnyama kunyolewa pale Temeke saa 24 zilizofuata watani wao Yanga walikuwa wakiingiza timu yao uwanjani dhidi ya moja kati ya timu chache bora zaidi barani Afrika, Mamelodi Sundowns. Saa moja kabla ya pambano kuanza kikosi kilipotangazwa ilishangaza zaidi.

Hakukuwa na mchezaji bora wa hatua ya makundi ya michuano hii, Pacome Zouzoua. Hakukuwa na jina la Khalid Aucho. Hakukuwa na jina la Yao Kouassi. Kifupi Yanga walimkosa beki bora wa kulia nchini. Wakaikosa injini yao ya kutuliza timu. Halafu mbele wakamkosa ‘bwana mipango’.

Sijui wangekuwepo kingetokea nini katika mipango ya kocha, Manuel Gamondi lakini ni wazi kwamba mpango kazi tuliouona wa kocha Gamondi ulikuwa ni kukaa chini na kuwaheshimu Mamelodi. Hakutaka kupishana no.

Kwa kiasi kikubwa iliwasaidia Yanga. Wakati mwingine unapima ubora wa wapinzani na kuamua namna ya kucheza. Hauchezi kwa ubora wako. Unacheza kutokana na ubora wa wapinzani wao. Unaweza kuwa mbabe wa soka la ndani. Lakini hauwezi kuwa bora dhidi ya Mamelodi.

Timu kubwa ambayo imeanza kutupa kiburi cha kupishana nao ni Al Ahly. Wengine ni Wydad Casablanca. Lakini kumbe kwa mawazo ya Gamondi ni kwamba Mamelodi hatuna kiburi cha kupishana nao. Ni kweli iliwasaidia Yanga.

Jonas Mkude aliwashangaza watu kwa kuchukua nafasi ya Aucho na yeye akafanya kazi ya kuziba njia. Dickson Job alionekana kuwa mwafaka kucheza katika ulinzi wa kulia kuliko Kibwana Shomari. Naye akaziba njia.

Kulikuwa na uwiano mzuri wa kuzuia kutoka kwa watu wa mbele kina Clement Mzize, Maxi Nzengeli na wengineo. Mudathir Yahya hakuwa yule tunayemjua katika siku za hivi karibuni ambaye amekuwa mwepesi katika kulichungulia lango la adui.

Akatumia muda mwingi kukaa nyuma na Mkude.

Pamoja na ukweli kwamba Mamelodi walipata umiliki mwingi wa mpira lakini takwimu nyingine zilizobaki hazikuwa mbaya kwa Yanga. Kwa mfano, Masandawana walipiga mashuti mawili tu yaliyolenga lango wakati Yanga ilipiga mashuti manne yaliyolenga lango. Hiki kilikuwa kiashiria kwamba Yanga walikuwa wameziba njia za Mamelodi.

Lakini hapo hapo Mzize angekuwa makini Yanga wangeweza kuiba ushindi wa ajabu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Alipata nafasi ya kutazamana na kipa wa Mamelodi, Ronwen Williams (32), lakini akashindwa kutumia mwanya huo vema. Ilikuwa nafasi ya wazi.

Mara nyingi makocha wanaosifika kucheza kwa mbinu nzuri za kujilinda ni Waitaliano. Kwa Argentina kocha ambaye amekuwa akisifika kucheza kwa mbinu hizi ni Diego Simeone wa Atletico Madrid. Kumbe kuna Muargentina mwingine ambaye ana uwezo wa kucheza hivi. Gamondi.

Na sasa Ijumaa hii kutakuwa na pambano la marudiano pale Pretoria. Wataanza Yanga na Mamelodi usiku wa saa tatu na kisha saa tano usiku pale Cairo kutakuwa na pambano la Simba na Al Ahly. Hili la Simba tulilizungumzia jana. Hili la Yanga nalo litakuwa pambano la kifo.

Kuna nadharia mbili hapa. Yanga wanaamini kwamba wana nafasi ya kushinda na kupita kwa sababu wameshawahi kufanya hivi msimu uliopita dhidi ya klabu mbalimbali na Afrika.

Unaweza kuwa ulifika katika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini zipo nyakati unapima ubavu wako na kujua wazi kwa kuzihesabu kwa vidole. Walifanya dhidi ya Rivers, dhidi ya Marumo, dhidi ya Club Africain, walifanya dhidi ya El Marreikh na wengineo.

Na katika kuamini huku pia wanaamini kwamba kurudi uwanjani kwa Aucho na Pacome kutawasaidia zaidi. Naambiwa kwamba Yao atakosekana kwa sababu atakuwa nje kwa muda mrefu zaidi kuliko wenzake kwa mujibu wa ratiba ya daktari.

Wakati Yanga wakiwa wanashangilia sare wakiamini kwamba hayakuwa matokeo mabaya dhidi ya Mamelodi tunataka kujua kama kile kilikuwa ni kiwango cha mwisho cha Mamelodi au kama wanaweza kufanya zaidi ya pale wakiwa kwao Afrika ya Kusini. Wataongeza nini zaidi? Kasi au? Ni suala la kusubiri Ijumaa usiku.

Hata hivyo, kuna kitu cha kushangaza kidogo. Wakati mwingine Mamelodi inaonekana kuogopwa kuliko Al Ahly na wakubwa wengine wa Afrika wakati rekodi yao sio ya kutisha. Inazungumzwa kwa ukubwa kama vile wamekuwa wakichukua taji hili mara nyingi kama ilivyo kwa kina Al Ahly.

Ukweli uliopo ni kwamba Mamelodi wamechukua taji hili mara moja tu chini ya Pitso Mosimane mwaka 2016. Na walifika fainali nyingine mwaka 2001 lakini wakafungwa. Hii inamaanisha kwamba Mamelodi hizi ni hatua pia ambazo amekuwa akiishia.

Kwa misimu mitano mfululizo Simba imekuwa ikiishia robo fainali ya michuano hii kumbe imekuwa ikipitwa hatua moja tu na Mamelodi ambao huwa wanakwenda kuishia nusu fainali au robo fainali kama wao. Huwa sifa za Mamelodi zimekuwa kubwa kuliko hali halisi.

Takwimu zao haziendi sambamba sana na sifa ambazo wamekuwa wakipewa na mashabiki wa Tanzania. Labda inatokana na kichapo kikali cha mabao 5-0 ambacho waliwapa Al Ahly katika michuano hii miaka michache iliyopita.

Itakuwa mechi ya kufa au kupona kwa Yanga. Kama wataweza kuziba njia tena na kuongeza umiliki wa mpira kupitia kwa Aucho halafu wakaongeza ubunifu katika eneo la mwisho kupitia kwa Pacome huenda wakapata kitu kwenye uwanja wa ugenini.

Litakuwa pambano la machozi, jasho na damu. Nafuu pekee ambayo Yanga wanaweza kuwa nayo dhidi ya Simba ni ukweli kwamba hawatakuwa wanacheza katika ardhi ya Waarabu. Walau mashabiki wa Mamelodi wanaweza kuwapa unafuu wachezaji wa Yanga kuliko mashabiki wa Mafarao ambao tunawajua kwa vurugu zao. Kila la kheri Simba na Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: