Ni rasmi sasa kwamba Miguel Gamondi atasalia Yanga msimu ujao. Mwanaspoti linajua kwamba amejilipua na mastaa wanne ambao ana uhakika watamuongezea kitu.
Mwanaspoti linajua kwamba viongozi wamemhakikishia asilimia zote kwamba watanunua mastaa wapya wanne sokoni kwenye dirisha hili ili kuja kivingine msimu ujao.
Habari za ndani zinasema kwamba miongoni mwa mambo ambayo alikuwa akihofia Gamondi ni kama ataweza kupata mafanikio zaidi ya yale ya msimu huu kwa aina ya kikosi alichonacho.
Lakini Mwanaspoti pia linajua kwamba atapukutisha mastaa wanne wa kigeni kwenye kikosi cha sasa ambao ni Skudu Makudubela, Agustine Okrah, Joyce Lomalisa na Kennedy Musonda.
Habari za uhakika zinasema kuwa mabosi wa Yanga wamemhakikishia usajili wa maana Gamondi ambao watakuja kubadilisha mambo kwenye kikosi cha kwanza na miongoni mwao ni beki Chadrack Boka wa FC Lupopo ya DR Congo. Ingawa na Clatous Chama anatajwa sana.
Mkataba mpya wa Gamondi, utamuweka kwenye presha kubwa ya kutakiwa kwanza kuchukua mataji manne ya ndani Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB, Kombe la Muungano pamoja na ngao ya hisani inayoanza Agosti.
Hata Kombe la Cecafa nalo litamhusu kocha huyo anayevizia tuzo ya kocha bora kwa msimu uliopita.
Kimataifa sasa baada ya Yanga kufikia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mabosi wa Yanga wamembana Gamondi wakimtaka afike hatua ya nusu fainali kama si kucheza fainali ya mashindano hayo kwa msimu ujao.
MZIGO MZITO
Ingawa mabosi wa Yanga hawakutaka kuweka wazi wala Gamondi mwenyewe lakini kocha huyo ameongezewa fedha ndefu zaidi ya mkataba wake utakaomfanya kuwa kocha anayelipwa zaidi hapa nchini.
Mbali na fedha hizo za mshahara Yanga pia imeboresha maisha ya nje ya kazi kwa kocha huyo ikimpokonya gari aina ya Rav 4 Toyota Vanguard na sasa atapewa gari ya kisasa zaidi.
MSIKIE GAMONDI
Akizungumzia mkataba huo Gamondi alikiri kwamba malengo ambayo amewekewa yatakuwa makubwa na kwamba haikuwa rahisi kwake kukubaliana nayo kirahisi kutokanana mafanikio ambayo waliyafikia msimu uliomalizika.
“Haikuwa rahisi unajua kuna sehemu ambayo tumefikia msimu huu, hapa maana yake unapokubali kubaki unatakiwa kuhakikisha msimu ujao unakwenda mbali zaidi ya hapa ulipoishia,”alisema Gamondi ambaye ni raia wa Argentina.
“Unatakiwa kuamua wewe kubaki hapo au kutafuta changamoto mpya lakini kama utabaki unatakiwa kujiuliza ni mambo gani ambayo yataifanya kazi yako kuwa rahisi kwa msimu ujao.
“Sote tunafahamu ugumu wa ligi ya hapa ulivyo, kitu kilichonivutia ni aina ya maboresho ambayo tutakwenda kuyafanya kwa msimu ujao, nadhani tutakuwa na timu bora zaidi kama haya ambayo tumeongea yatafanikiwa kukamilika, kila timu itakuja na nguvu ya kutaka kuzuia mafanikio yetu.”
MASHARTI KWA KINA PACOME
Akizungumzia mapumziko ya mwezi mmoja ambayo amewapa wachezaji wake, Gamondi alisema kila mchezaji amekwenda kwao akiwa na programu maalum ambayo anatakiwa kuhakikisha anaitekeleza na kila moja inatokana na ufanisi wa staa husika.
“Kila mchezaji anatakiwa kupumzika lakini hatuwezi kwenda kupumzika moja kwa moja kila mchezaji aliyemaliza msimu hapa amepewa ratiba ambayo anatakiwa kuitekeleza na kila wakati atawasilisha kwa kocha wa mazoezi (Taibi Lagrouni).
“Hili ni muhimu sana kwa kila mchezaji kuzingatia kinyume na hapo tutakuwa wakali kwa lengo la kutokuwa na kazi ngumu kwenye maandalizi ya mwanzo wa msimu, nimeambiwa muda hautakuwa wa kutosha sana lazima tujipange,”aliongeza Kocha huyo ambaye alikuwa akihusishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.