Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi aivimbia Yanga, ataka kuondoka

Yanga Gamondi Dodoma.jpeg Miguel Gamondi

Wed, 5 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa Yanga chini ya Rais wa timu hiyo, Injinia Hersio Said umeendelea kufanya vikao na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi aliyemaliza mkataba ili asalie kikosini, huku Muargentina huyo akipiga hesabu za kuondoka kwenda kutafuta changamoto nje ya klabu hiyo.

Yanga ilimsainisha Gamondi mkataba wa msimu mmoja akichukua mikoba ya Mtunisia Nasredine Nabi na sasa inahaha kuhakikisha inamuongezea mkataba kutokana na mafanikio aliyoipa timu hiyo, lakini hadi tunaingia mitamboni kocha huyo alikuwa hajamwaga wino, huku akihusishwa na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Mwanaspoti limejiridhisha Gamondi ana ofa nyingine nyingi nje ya Tanzania, lakini anapanga kubadili mazingira ya kazi baada ya Yanga licha ya kwamba bado hajafanya maamuzi ya moja kwa moja.

Baada ya mechi ya fainali kati ya Yanga na Azam iliyomalizika kwa Wanajangwani kutwaa ubingwa kwa mikwaju ya penati 6-5 kutokana na dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa suluhu, Gamondi aliwaaga mashabiki wa Yanga na kusema;

"Makocha tunapita. tunachotaka kufanya ni kuacha alama muhimu kwa klabu na kufikia mafanikio," alisema Gamondi katika mahojiano ya wazi na wanahabari na kungeza;

"Nataka kufikiri na kujadili kwani mkataba wangu unamalizika leo (juzi)." Hata hivyo, Mwanaspoti lilienda mbali na kumtafuta kocha huyo kumuuliza kuhusu ofa aliyonayo kutoka kwa Kaizer Chiefs na timu nyingine na kukiri kuwepo na mazungumzo lakini hakuweka wazi kama tayari amesaini mkataba wa awali na wakali hao wa Afrika Kusini au timu nyingine tofauti na Yanga.

Gamondi alisema kwa kuwa kazi yake ni ukocha basi anaweza kufundisha timu na baadae kuondoka kwenda sehemu nyingine anayoona anaweza kufanya nayo kazi hivyo hajui msimu ujao atakuwa akiifundisha timu gani.

“Makocha tunaajiriwa na kufukuzwa, kama nikiondoka hapa (Yanga) naamini nitapata timu nyingine na nitafanya vizuri na kufukuzwa pia, bila kujali nimeondoka vipi,” alisema Gamondi.

Aidha kocha huyo aliyeipa Yanga mafanikio kwa msimu huu ikiwemo taji la ligi Kuu, kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza na kutwaa taji la FA alisema mafanikio hayo aliyoyapata ndani ya timu hiyo ni kutokana na maandalizi imara.

"Bila maandalizi mazuri tusingepata matokeo mazuri ambayo leo hii yamemfurahisha kila mmoja wetu, namshukuru kila mmoja kwenye timu hii bila kuwasahau mashabiki ambao wamekuwa wakitusapoti kila tunapokuwa," alisema.

YANGA INAPAMBANA

Licha ya kwamba mawazo ya kocha huyo ni kuondoka Yanga msimu huu, lakini bado viongozi wa timu hiyo wanaendelea kupambana kuhakikisha wanampa mkataba mpya.

Moja ya vigogo wa timu hiyo (jina tunalo), aliliambia Mwanaspoti bado Yanga haijakata tamaa kuhusu kumbakisha kocha huyo lakini ni jambo ambalo linazidi kuwa gumu.

"Yanga ina mpango na Gamondi. Tulimuita na kuongea naye kuhusu mkataba mpya mapema tu lakini alituambia tumpe muda ili amalize msimu kisha tutazungumza.

Tunajua kuna timu zimempa ofa nzuri ila tunapambana nazo kuhakikisha tunashinda vita hii," alisema kiongozi huyo. Aidha Mwanaspoti lilidokezwa kocha huyo kuna baadhi ya vitu vinampa ugumu kuongeza mkataba ndani ya Yanga ikiwemo vipengele alivyowekewa kwenye mkataba mpya.

Inaelezwa miongoni mwa malengo ambayo kama Gamondi atasaini mkataba mpya ndani ya Yanga atatakiwa kuyatimiza ni pamoja na kuifikisha timu hiyo nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na kutetea mataji yote ya ndani ikiwemo lile la ligi. Gamondi anataka kujiweka pembeni katika presha hiyo huku akiamini anahitaji changamoto mpya nje ya Yanga.

Jana Jumatano, Yanga na Gamondi walitarajiwa kukutana katika kikao cha mwisho ambacho kitaamua hatma ya kocha huyo kama ni kusalia Jangwani ama kuondoka.

Hata hivyo, huenda dili la Gamondi na Kaizer Chiefs likafa kutokana na Wasauzi hao kuwekeza nguvu zaidi kwa Nabi ambaye kwa sasa anainoa Far Rabat ya Morocco na kama hilo lisipokamilika basi Yanga itakuwa na nafasi kubwa ya kumbakiza kocha huyo kutokana na ofa nyingine alizonazo kutajwa kuwa za kawaida.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: