Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi aichambua Yanga mpya

Gamondi Kambi Gamondi aichambua Yanga mpya

Tue, 25 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kuiongoza timu yake katika mechi ya kwanza ya kirafiki kwa mara ya kwanza tangu aanze kuinoa, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Angel Gamondi, ameeleza kufurahishwa na kiwango kizuri kilichooneshwa na wachezaji kwenye mchezo huo dhidi ya  Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi, ukiwa maalum kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wao kwenye Kilele cha Siku ya Mwananchi, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Kennedy Musonda baada ya pasi murua kutoka kwa Max Pia Nzengeli.

Baada ya kukamilika kwa dakika 90, Gamondi alisema alichoangalia zaidi ni muungano wa wachezaji wake na matokeo ilikuwa si muhimu sana kwake kwa sababu hakuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi.

Alisema alikuwa na siku 10 za maandalizi kwa sababu ya kuchelewa kujiunga kwa wachezaji wapya kutokana na usajili wa nyota hao kuchelewa.

“Hatukuwa na muda mrefu kwenye maandalizi, lakini nafurahi kuona wachezaji wamekuwa na muunganiko mzuri, tumetengeneza nafasi tatu tumekosa na kupata moja na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

"Mechi hii ni kipimo kizuri kwangu kwa kuwa nimeona ubora na madhaifu ya timu yangu, wapi natakiwa kufanyia kazi, ilikuwa mechi nzuri ya mbinu na ufundi kwa kila timu,” alisema Gamondi.

Kuhusu wachezaji wapya, alisema ameona muunganiko mzuri wa nyota hao na waliokuwapo tangu awali kwa kuonesha soka la kuvutia licha ya kwamba bado kuna mapungufu anatakiwa kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Naye Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs, Molefi Ntseki, alisema mechi hiyo ilikuwa kipimo kizuri kwa timu zote mbili, kiufundi na mbinu na kila mmoja amenufaika.

Alisema timu zote zilicheza vizuri na ameona mapungufu ya kikosi chake hivyo anakwenda kuyafanyia kazi kwa sababu amepata kipimo kizuri cha maandalizi ya msimu mpya.

“Japo wamepoteza, lakini nimefurahi kupata mechi dhidi ya Yanga ambayo imenipa mwanga wa mapungufu ya kikosi changu na timu zote zimecheza vizuri,” alisema kocha huyo.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema hatima ya wachezaji wanne ambao hawakutambulishwa katika Kilele cha Siku ya Mwananchi, wataiweka wazi hivi karibuni.

Yanga juzi walikamilisha tamasha lao  kwa kusherehekea Kilele cha Siku ya Mwananchi kwa kutambulisha nyota 26 ambao watakuwapo kwenye kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa 2023/24.

Katika utambulisho huo, Yannick Bangala, Djuma Shaaban na Mamadou Doumbia hawakuwapo kwenye orodha pamoja na Fiston Mayele, ambaye inaelezwa tayari ametimkia kunako Klabu ya Pyramids ya Misri.

“Kuhusu ‘THANK YOU’, hili itaendelea baada ya kamati itakapokutana na kufanya tathmini pamoja na kuweka wazi hatima ya wachezaji wetu wengine,” alisema Kamwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: