Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi afunguka kila kitu Yanga

Gamondi Miguel Tizi Gamondi afunguka kila kitu Yanga

Fri, 29 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Miguel Gamondi aliyekuwa sehemu ya benchi la ufundi la Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wakati likitwaa ubingwa wa saba wa Ligi Kuu ya nchini humo msimu wa 2005/06, amefichua kuujua mpango wa wababe hao, hivyo ameeleza na mkakati wa kuwasapraizi kesho Jumamosi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamani Mkapa.

Kocha huyo wa Yanga, ameeleza hilo kwenye mahojiano maalumu aliyoyafanya na mtandao wa CAF katika wiki hii ya kihistoria katika soka la Tanzania kwa timu mbili kucheza kwa pamoja hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Simba itashuka usiku wa leo Ijumaakutupa karata yao ya kwanza dhidi ya Al Ahly kabla ya kesho kuwa zamu ya vijana wa Jangwani dhidi ya Masandawana. Mtaalamu huyo wa ufundi, amesema hii ni vita ya wachezaji 11 kwa 11, hivyo licha ya uzoefu ambao Mamelodi wapo nao kwenye michuano hiyo, wapo tayari kuufanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi kwa wapinzani wao kwa namna ambavyo wamewasoma.

"Sundowns ni moja ya timu kubwa zinazofanya vizuri Afrika pamoja na Al Ahly, bila shaka ni bora zaidi. Wako hapo walipo leo kwa sababu ya uthabiti ambao wameonyesha kwa miaka mingi. Napenda sana mtindo wa uchezaji wa Sundowns. Wanacheza aina yao ya soka ninayoipenda. Nilikuwa kocha wa Sundowns na najua wanachopenda kufanya na kile wanachojenga sasa sio tu muhimu kwa Afrika Kusini, lakini kwa Bara la Afrika," amesema kocha huyo na kuongeza;

"Kwetu sisi (Yanga), labda atakuwa mpinzani mgumu zaidi kukabiliana naye lakini tupo tayari kumfanya ateseke (kumpa wakati mgumu) wakati huo huo itakuwa ni uzoefu mzuri wa kujifunza kwani tunacheza na timu yenye ubora na ufundi wa hali ya juu. Nadhani huu utakuwa mchezo bora wa kuutazama."

Kuhusu mpango wa kuvuka robo fainali, licha ya kukiri kuwa na kibarua kizito, Gamondi amesema; "Lengo la klabu ilikuwa ni kufika hatua ya makundi na baada ya kufikia hilo, tukasema tunataka kushindana na kushinda dhidi ya klabu kubwa kama Ahly."

"Tunataka kufanya vizuri katika mtoano kwani itakuwa tathmini nzuri ya mahali tulipo. Ni uzoefu wa kujifunza na kwa hakika, tutacheza bora tuwezavyo. Huenda tusiwe katika hali nzuri zaidi kwa mchezo huu kwa vile baadhi ya wachezaji walirejea wakiwa na majeraha kutoka kwa mapumziko ya FIFA, ila tutajaribu tuwezavyo na kuonyesha kwamba tunastahili kuwa katika hatua hii ya mashindano."

Gamondi ameongeza kwa kusema, "Katika soka huwezi jua. 'Logic' inasema Sundowns ndio timu kubwa na wamecheza kwa muda mrefu pamoja na kuwekeza pesa nyingi, lakini mpira wa miguu ni 11v11 na tunatumai kuwa tutapata matokeo. Sisi ni timu ya ushindani, na tutafanya tuwezavyo."

TIMU MBILI ROBO

Kocha huyo, ameiongelea wiki hii kama ya kipekee na kihistoria kwa kusema; "Ni mara ya kwanza wote wawili kufika robo fainali kwa pamoja. Hii inaonyesha uboreshaji mkubwa katika usimamizi wa klabu. Unaweza kuona wamejitolea kuboresha na kuleta ubora."

"Tunatumani kuwa matokeo yanaweza kutoa motisha zaidi kwa usimamizi na shirikisho letu kujenga miundombinu zaidi na kuunda uwezekano zaidi wa maendeleo ya vijana. Nchi hii ina uwezo mzuri, na hili ni muhimu kwa soka la Tanzania. Ninaamini wiki hii itaweka jina la soka la Tanzania midomoni mwa wengi kupitia mashindano makubwa ya klabu," alifafanua Gamondi na kuongeza;

"Nimefurahishwa sana na yaliyotokea katika nchi hii katika miaka miwili iliyopita."

YANGA INABEBA TENA

Kuhusu mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Gamondi amesema; "Kufikia sasa ni nzuri sana. Tuko juu ya msimamo. Kilicho muhimu ni kuendelea kucheza kwa mtindo mzuri wa kututambulisha. Ni muhimu kuwapa furaha mashabiki wetu kwa sababu katika nchi mashabiki wetu wamekuwa wakituunga mno mkono hata awamu ambazo huwa tunateleza."

"Tunajaribu kufanya tuwezavyo na kila wakati kupata matokeo ambayo ni muhimu. Natumai tunaweza kuendelea kufanya vizuri hadi kushinda ligi tena.

Gamondi aliyeajiriwa mwishoni mwa msimu huu akichukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyekuwa amemaliza mkataba, ameiongoza timu hiyo kuweka rekodi kadhaa klabuni hapo na kwa soka la Afrika ikiwamo kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kupita miaka 25 tangu ilipocheza mwaka 1998.

Katika kutinga hatua hiyo, Gamondi aliiduwaza Al Merrikh ya Sudan ambayo ilikuwa haijawahi kupoteza mechi dhidi ya Yanga kwa kufungwa nje ndani jumla ya mabao 3-0 na kutolewa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga ilishinda 2-0 katika mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Kigali, Rwanda kisha kushinda 1-0 nyumbani, lakini akiivuka kutoka makundi kuingia robo kwani haikuwahi kutokea kwa Yanga tangu michuano hiyo ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika na kuwa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1997.

Kwa upande wa Ligi, ameiongoza timu hiyo kukaa kileleni ikiwa na pointi 52 kupitia mechi 20, huku ikitoa dozi za tano tano kwa wapinzani ikiwamo Simba iliyowanyoa 5-1 katika Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana mbali na 5-0 dhidi ya JKT TZ, Ihefu na KMC.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: