Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Miguel Gamondi, amebainisha kwamba, hali ya kikosi ipo vizuri katika kuelekea mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Ijumaa ya wiki hii kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld uliopo Pretoria, Afrika Kusini, kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Tanzania, baada ya ule wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam, matokeo kuwa 0-0.
Gamondi amesema: “Tupo salama, tumefanya mazoezi yetu ya kwanza hapa Pretoria ya kuweka miili sawa kutokana na safari, tuna fuaraha, tupo katika hali nzuri, kesho (leo Jumatano) tutaanza mazoezi yenyewe kabisa.
“Timu ipo vizuri, tunafanya mazoezi na wachezaji waliokuwa majeruhi (Pacome, Aucho, Yao), siku zote tunapaswa kuamini na kufanya kwa juhudi kubwa, hicho ni kitu muhimu sana.
“Ukweli nina kundi la wachezaji wazuri ambao wanafanya mazoezi kwa nguvu, wapo makini, Jumamosi pale Uwanja wa Benjamini Mkapa walionesha ukomavu wa kweli.
“Ninawatakia Wananchi safari njema wanapokuja hapa, nawapa hongera kwa kutusapoti. Ninaamini watafika salama kabisa.”