Kocha Mkuu wa Yanga, Muargentina Miguel Gamondi ameuambia uongozi wa timu hiyo kuwa lazima wasajili straika wa kigeni mwenye uwezo na uzoefu atakayekiongozea nguvu kikosi hicho katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kauli hiyo imekuja zikiwa zimebakia siku tano kabla ya usajili wa dirisha dogo alijafungwa Januari 15, mwaka huu Yanga ikiwa imekamilisha usajili wa wachezaji wawili pekee Shekhan Ibrahim na Augustine Okrah pekee.
Wachezaji hao tayari wamejiunga na timu hiyo, wakicheza michezo ya Kombe la Mapinduzi kabla ya kutolewa hatua ya Robo Fainali dhidi ya APR ya nchini Rwanda.
Mmoja wa Mabosi wa Yanga Championi Ijumaa, Gamondi amewaambia viongozi wa timu hiyo, kuwa anataka mshambuliaji ambaye muda wote anacheza eneo la ndani ya 18 la goli la timu pinzani, na siyo anayetoka eneo hilo.
Bosi huyo alisema kuwa, lengo la kutaka straika wa aina hiyo, ni kutokana na uwepo wa viungo wengi wenye uwezo kutengeneza nafasi nyingi za kufunga baadhi ni Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Stephen Aziz Ki.
Aliongeza kuwa straika huyo anayekuja ni suala la muda pekee la kutangazwa, ni baada ya kumaliza mazungumzo ya awali ya kumsajili katika dirisha hili dogo na kati ya hao anayetajwa ni mshambuliaji Glody Kilangalanga raia wa DR Congo.
“Hatutaki kubahatisha katika usajili wetu wa mshambuliaji wa kati, kikubwa kocha ametoa mapendekezo yake ya aina ya mshambuliaji anayemtaka katika dirisha dogo.
“Kikubwa anataka mshambuliaji mwenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa, atakayekuja kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, katika dirisha dogo.
“Sifa nyingine kubwa ambayo kocha ameitoa anataka kuwa nayo mshambuliaji ni yule ambaye muda wote anakuwepo ndani ya 18 ya goli la timu pinzani, kwani anao viungo wengi wenye uwezo wa kutengeneza nafasi za mabao,” alisema bosi huyo.
Juzi Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Bado hatujamaliza usajili katika dirisha dogo, bado kuna maingizo ya mapya yanakuja akiwemo mshambuliaji mmoja wa kati, na muda wowote utakamilika usajili wake.”