Kocha Mkuu wa Yanga, Muargentina, Miguel Gamondi anasuka kikosi chake kwa ajili ya mechi zijazo ikiwemo ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merrikh ya Sudan.
Mchezo huo utakaopigwa Septemba 16 mwaka huu, jijini Kigali huku akijiandaa kuwasapraizi wapinzani hao kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Timu hizo zitakutana kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kurudiana wiki moja na mshindi wa jumla kutinga makundi, huku kocha Gamondi akifahamu Wasudani wameshampiga chabo amepanga kwenda kuwasapraizi ugenini akipanga kumtumia winga Msauzi, Mahlatsi Makudubela ‘Skudu’ aliyerejea uwanjani tangu alipoumia mwezi uliopita kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.
Gamondi anayesifika kwa mbinu tofauti na uwezo mkubwa wa kufanya mabadiliko wakati mchezo ukiendelea na kwenye mechi tofauti alithibitisha kupona kwa Skudu na kuwa tayari kwa mechi lakini wikiendi hii Yanga itacheza mechi ya kirafiki itakayokuwa mtihani wa mwisho kwa Skudu kabla ya kupewa Merriekh.
“Skudu yuko vizuri na amefanya mazoezi yote na timu kwa ufasaha mkubwa. Ni miongoni mwa wachezaji ninaopanga kuwatumia kwenye Ligi ya Mabingwa, lakini kwa sasa tunatarajia kuwa na mechi ya kirafiki wikiendi hii ambayo itanipa picha kamili ya kikosi kizima na utayari wa Skudu kucheza,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Kila mchezaji wa Yanga ana nafasi kikosini hivyo napenda kuwaona wote wakiwa timamu kwani wanatupa matumaini na wigo mpana wa kupanga kikosi kwenye mechi.”
Skudu alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Marumo Gallants ya Afrika Kusini, tangu atue amecheza mechi mbili tu, ya Wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs na ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC aliyoumia dakika ya saba na kushindwa kuendelea na mchezo huo.
Baada ya hapo Yanga ilicheza mechi tano za kimashindano bila Skudu, moja ikiwa ni fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, mbili za Ligi Kuu na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali jambo linalowafanya mashabiki wa Yanga kuwa na shauku ya kumuona mkali huyo wa chenga na kuchezea mpira.
Baada ya mechi ya kirafiki, Yanga itaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya Septemba 14 kusafiri hadi Kigali, Rwanda kwa mchezo wa kwanza na Al Merrikh katika mchezo wa kwanza kabla ya marudiano utakaopigwa Septemba 29.