Yanga iko Misri ikijiandaa na mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha wake, Miguel Gamondi ametoa ya moyoni.
Amewaambia wachezaji wake kwamba kiwango ambacho wamekionyesha kwenye mchezo uliopita ndicho ambacho anataka timu yake iwe nacho.
Yanga iliupiga mwingi kwenye mchezo wa nyumbani dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria ikishinda kwa kishindo cha mabao 4-0 huku ikitinga hatua ya robo fainali na sasa inacheza mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya bingwa mtetezi Ahly itakayopigwa Machi 2.
Gamondi ameliambia Mwanaspoti kuwa baada ya wiki chache za kikosi chake kurejea kuwa pamoja kufuatia kumalizika kwa fainali za Mataifa Afrika mechi hiyo dhidi ya Belouizdad imethibitisha kurejea kwa ubora ambao waliuanza mwanzoni.
“Uwezo ambao tumeuonyesha dhidi ya CR Belouizdad hicho ndicho kiwango ambacho falsafa zangu zinataka tucheze. Tulicheza mpira mkubwa. Kilikuwa ni kiwango ambacho kama sio kusimama kwa ligi tulitakiwa kukifikia muda mrefu,” alisema Gamondi ambaye ni raia wa Argentina.
“Nimewaambia wachezaji wangu tunatakiwa kushika hapa na kuendelea kucheza kwa kiwango hiki zaidi. Tukifanikiwa hilo hakuna ambacho kitazuia mafanikio yetu kwenye malengo yetu. Hatupaswi tena kucheza chini ya hapa.”
Gamondi alisema faida kubwa kwa wachezaji wake ni kwamba aina ya mazoezi ambayo wanayafanya yanawapa nafasi ya kucheza kwenye ubora huo ambao waliuonyesha kwenye mechi iliyopita.
Hata hivyo, kocha huyo alisema kitu pekee ambacho wanatakiwa kupambana nacho ni utumiaji wa nafasi nyingi ambazo wanatengeneza uwanjani kwenye mechi mbalimbali wanazocheza.
“Tunahitaji kujipa utulivu wa kutumia nafasi za uwanjani.
Tunatengeneza nafasi nyingi na nyingi zinapotea. Mbaya ziada ni zile ambazo hutarajii kuona tunazikosa. Nafahamu huwezi kutumia nafasi zote lakini ni vyema kama unaweza kufunga zaidi unafanya hivyo,” alisema.
Katika msimu huu Yanga ikiwa chini ya Gamondi imeshinda mechi 16 zikiwemo 14 za ligi ya ndani huku mbili ni za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ikitoka sare tatu ambapo mbili ni Ligi ya Mabingwa na moja ya ligi ya ndani na kupoteza mechi mbili pekee moja kwa kila mashindano hayo mawili.
Yanga ndio timu iliyofunga mabao mengi kwenye kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ikifunga tisa, lakini pia ikiruhusu mabao matano kwenye mechi tano huku kwe-nye ligi ya nyumbani ikiwa imekabana na Azam FC - zote zikiongoza kwa kufunga mabao 39.