Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi, Yanga mambo bado magumu

Hersi X Gamondi Usajili Miguel Gamondi na Injinia Hersi

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mambo bado baina ya kocha Miguel Gamondi na mabosi wa Yanga baada ya kushindikana kukutana juzi Jumatano ili kujadiliana juu ya mkataba mpya na sasa kocha huyo anaendelea kula zake bata visiwani Zanzibar wakati anasikilizia simu za kuitwa jijini Dar es Salaam.

Gamondi amemaliza mkataba aliokuwa nao na Yanga baada ya kuiwezesha kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo na tayari ana ofa za kutosha mezani huku mabosi wa klabu hiyo wakimpigia hesabu wambakishe waendelee pale walipoishia.

Sasa unaambiwa jana Jumatano kocha huyo alikuwa akisikilizia simu iite kutoka kwa mabosi wa Yanga ili waende kukutana mezani kujadili dili jipya kutokana na mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika.

Hata hivyo, kitu cha ajabu ni kwamba simu ya Gamondi iliita mapema tu, lakini taarifa aliyopewa ilikuwa tofauti na aliyotarajia kwani aliambiwa hivi;

"Asubuhi hii tunaenda kwa wadhamini wetu kuna shughuli kidogo, tutazungumza jioni tukitoka huko." Hiyo ilikuwa ni sauti inayodaiwa ilisikia masikioni mwa Gamondi kutoka kwa kigogo mmoja wa juu wa Yanga akimpa taarifa Muargentina huyo.

Yanga jana Jumatano walikuwa na shughuli ya kupongezwa na wadhamini wao wakuu SportPesa kutokana na mafanikio waliyotapata msimu huu ikiwemo kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kushinda kombe la Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho, vigogo wa timu hiyo walipanga kukutana na Gamondi jioni lakini ilishindikana.

Mtu wa karibu na kocha huyo, ameliambia Mwanaspoti kwamba hakukuwa na mazungumzo yoyote hivyo bado Gamondi anawasikilizia mabosi wa Yanga huku akiwa zake mapumziko visiwani Zanzibar.

"Baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam kocha Gamondi hakurudi Dar, alibaki Zanzibar kwa ajili ya mapumziko, lakini aliwaambia mabosi wa Yanga kwamba wafanye mazungumzo ya hatma yake kabla hajasepa kurudi kwao.

"Jana Jumatano ndiyo walipanga kuzungumza lakini ilishindikana baada ya Yanga kualikwa na SportPesa kwenda kupongezwa," alisema mtu huyo.

"Kutokana na ratiba kuingiliana aliambiwa jioni baada ya shughuli hiyo kumalizika wanaweza kuzungumza lakini haikuwa hivyo. Kocha amebaki tu kuwasikilizia."

Muargentina huyo anapiga hesabu za kuondoka kwenda kutafuta changamoto nje ya klabu hiyo baada ya kuiongoza Yanga kwa msimu mmoja akichukua mikoba ya Mtunisia Nasreddine Nabi.

Yanga inapambana kuona inambakisha kocha huyo aliyefanya mazuri kwa kipindi kifupi huku akihusishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayotaka huduma yake.

Mwanaspoti limejiridhisha Gamondi ana ofa nyingine nyingi nje ya Tanzania, lakini anapanga kubadili mazingira ya kazi baada ya Yanga licha ya kwamba bado hajafanya uamuzi wa moja kwa moja.

Wikiendi iliyopita baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na Azam iliyomalizika kwa Wanajangwani kutwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 kutokana na muda wa kawaida mchezo huo kumalizika kwa suluhu, Gamondi aliwaaga mashabiki wa Yanga na kusema;

"Makocha tunapita. Tunachotaka kufanya ni kuacha alama muhimu kwa klabu na kufikia mafanikio," alisema Gamondi katika mahojiano ya wazi na wanahabari na kuongeza;

"Nataka kufikiri na kujadili kwani mkataba wangu unamalizika leo (Juni 2, 2024)."

“Makocha tunaajiriwa na kufukuzwa, kama nikiondoka hapa (Yanga) naamini nitapata timu nyingine na nitafanya vizuri na kufukuzwa pia, bila kujali nimeondoka vipi,” alisema Gamondi.

MGUU NDANI, MGUU NJE

Licha ya kwamba Gamondi amekaribisha mazungumzo na mabosi wa Yanga kuangalia hatma yake kama ataendelea au atasepa, lakini kuna baadhi ya vitu vinampa ugumu kuongeza mkataba ikiwemo vipengele alivyowekewa kwenye mkataba mpya.

Inaelezwa kati ya malengo ambayo kama Gamondi atasaini mkataba mpya ndani ya Yanga atatakiwa kuyatimiza ni pamoja na kuifikisha timu hiyo nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao sambamba na kutetea mataji yote ya ndani ikiwemo lile la ligi.

Gamondi anataka kujiweka pembeni katika presha hiyo huku akiamini anahitaji changamoto mpya nje ya Yanga.

Hata hivyo, huenda dili la Gamondi na Kaizer Chiefs likafa kutokana na Wasauzi hao kuwekeza nguvu zaidi kwa Nabi ambaye kwa sasa anainoa Far Rabat ya Morocco na kama hilo likikamilika basi Yanga itakuwa na nafasi kubwa ya kumbakiza kocha huyo kutokana na ofa nyingine alizonazo kutajwa kuwa za kawaida.

NINI KIFUATACHO

Ikitokea Gamondi amebaki au ameondoka, msimu ujao utakuwa wa tofauti sana kwa Yanga ambayo inahitaji mafanikio ya msimu uliomalizika yanakuwa juu zaidi.

Gamondi wakati anakabidhiwa mikoba ya Nabi kuinoa Yanga, alikuta timu hiyo ina mataji matatu ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho. Pia timu ikitoka kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hayo yote yalitokea 2022/2023.

Kocha huyo alianza kwa kupoteza Ngao ya Jamii mbele ya Simba, lakini akatetea mengine yaliyobaki huku akitoa bonasi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati malengo yalikuwa ni kutinga hatua ya makundi katika michuano hiyo.

Mzigo uliopo sasa ni kuona kocha wa msimu ujao iwe Gamondi au yeyote yule, lazima afikie malengo ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sambamba na kutetea mataji yao mawili na kubeba Ngao ya Jamii waliyoipoteza kwa Simba.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: