Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi: Yanga hii inacheza kibingwa

Yanga Gamondi Wachezaji Gamondi: Yanga hii inacheza kibingwa

Fri, 27 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kukiongoza kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema ameanza kuona dalili za ubingwa kutokana na kiwango bora kilichooneshwa na timu yake katika mchezo huo.

Yanga kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kufikisha pointi 15 sawa na Simba, lakini mabingwa watetezi hao wakiwa mbele kwa mchezo mmoja.

Akizungumza Kocha Mkuu wa Tumu hiyo, amesema wachezaji wake walionesha tabia halisi za timu bingwa na wanahitaji ubingwa msimu huu kutokana na kucheza kwa kujitoa na kutafuta pointi tatu licha ya kutanguliwa.

“Nilitarajia ugumu kwenye mchezo huo, wachezaji wangu wameonesha tabia halisi ya kwamba wapo kwenye timu kubwa inayohitaji ubingwa, tulicheza vizuri kipindi cha pili licha ya kutanguliwa bao la penalti, lakini tulipambana na kusawazisha makosa yetu na kuongeza,” alisema Gamondi.

Kocha huyo pia alimpongeza mfungaji wa mabao yote matatu Stephen Aziz Ki, akisema ni mchezaji wa daraja la juu mno kwani pamoja na uchovu aliokuwa nao, lakini alicheza kwa kujitoa kuipigania timu yake kitu ambacho kimeonesha ana mapenzi makubwa na timu hiyo.

Aidha, Gamondi alisema ushindi huo ulikuwa muhimu zaidi kwao katika kujiimarisha na kuongeza hamasa kuelekea michezo ijayo ya ligi hiyo.

“Ushindi ulikuwa muhimu sana, nashukuru tumetimiza malengo yetu japo haikuwa kitu rahisi, Azam walicheza vizuri na kuna muda waliuchukua mchezo,” alisema.

Alisema kwenye mbio za ubingwa ni timu inapopata ushindi dhidi ya timu zinazoonekana kuwa wapinzani wa karibu inajiweka katika mazingira mazuri kuelekea mwishoni mwa ligi.

“Sasa tunajipanga kwa michezo mingine ya mbele yetu, hatutaki kuangalia matokeo ya wengine, tunaangalia namna gani tunafikia malengo yetu,” alisema Gamondi.

Naye Kocha Msaidizi wa Azam FC, Bruno Ferry, alisema kilichowaangusha ni kushindwa kudhibiti mchezo baada ya kuongoza kwa mabao 2-1 kutokana na kukosa uzoefu kwa wachezaji wake, lakini ubora waliokuwa nao wachezaji wa wapinzani wao Yanga.

Alisema ulikuwa mchezo mkubwa uliokutanisha timu mbili kubwa na walijitahidi kupambana kwa kuushika katika baadhi ya nyakati, lakini ubora wa Yanga hasa kiungo Aziz Ki ndio uliwaletea shida na kujikuta wanapoteza mchezo.

“Naipongeza Yanga pamoja na Azizi Ki, alikuwa bora na ndiye amesababisha tukapoteza mchezo, lakini ndio mpira tunarudi kujipanga ili kufanya vizuri mchezo unaokuja lengo ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu,” alisema Ferry.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: