Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amewatuliza mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kwamba ana kikosi kizuri cha kushindana na Mamelodi Sundowns katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya uwajibikaji mzuri wa wachezaji wa timu katika mechi ya kwanza.
Yanga ilitoka suluhu na Mamelodi katika mechi ya kwanza iliyopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na tayari ipo Afrika Kusini kwa mechi ya marudiano itakayochezwa leo Ijumaa, ikihitaji sare yoyote ya mabao au ushindi kwenda nusu fainali.
Gamondi ameliambia Mwanaspoti akiwa Sauzi kwamba wanaendelea na maandalizi ya mchezo ujao akiwa tayari kwa vita kuwakabili Mamelodi.
"Tulifika jana na jioni yake tulifanya mazoezi mepesi jana Alhamisi tulifanya mazoezi magumu nashukuru Mungu baadhi ya wachezaji majeruhi wameanza mazoezi na wanaonyesha kuuhitaji mchezo wa leo Ijumaa," alisema Gamondi na kuongeza;
"Mimi ni muumini wa kuamini ushindi na sio kupoteza au kuwa na hofu nina wachezaji wazuri wenye uwezo wa kupambana na mpinzani wetu natarajia mchezo mzuri na wa ushindani huku nikiwa na imani kubwa ya kupata matokeo."
Gamondi alisema uwajibikaji walioufanya wachezaji wake kwenye mchezo wa kwanza unampa imani kubwa ya kufanya vizuri zaidi leo huku akiweka wazi kuwa wana faida kubwa kuto kuruhusu bao nyumbani.
''Wachezaji wapo kwenye hali nzuri na wana hali nzuri ya kuutaka mchezo wetu ujao naamini watapambana zaidi ya walivyofanya mchezo wa kwanza,'' alisema kocha Gamondi
Mara ya mwisho Mamelodi kupoteza mchezo wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani ilikuwa ni dhidi ya CR Belouizdad Aprili 2021, lakini imecheza mechi kadhaa za karibuni bila kupoteza na kwa michezo saba iliyopita ikiwamo ya Ligi Kuu na michuano mingine haijapoteza hata mara moja.
Katika mechi za makundi timu hiyo ilipoteza mechi moja tu ya ugenini dhidi ya TP Mazembe, mechi nyingine ikipata matokeo ya ushindi na sare na kufunga mabao saba na kuruhusu moja tu, huku Yanga mechi ya mwisho ya ugenini katika makundi ilipoteza mbele ya Al Ahly ya Misri.