Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi raia Argentina, amewaangalia wapinzani wake katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Merrikh ya Sudan, kisha akasema hawezi kuwa na presha ya kupata matokeo mazuri mbele yao kutokana na kikosi imara alichoachiwa na mtangulizi wake, Nasreddine Nabi.
Gamondi ametoa kauli hiyo kuelekea mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza dhidi ya AI Merrikh unaotarajiwa kupigwa Septemba 16, mwaka huu nchini Rwanda.
Gamondi amesema anachokiangalia kwa sasa ni kupata matokeo ya ushindi dhidi ya wapinzani wake hao na hana presha yoyote kufanikisha Young Africans kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kitu kikubwa kwa sasa ni kwamba tunaendelea kujenga timu ili kupata matokeo bora katika mchezo ujao dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, tunachokiangalia kwa ukubwa ni ubora wa wapinzani wetu kwa namna walivyo ingawa ninawaamini wachezaji waliopo kwenye kikosi changu.
“Unajua suala la uzoefu, sina presha nalo kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji wetu wameshacheza haya mashindano, wanajua nini ambacho tunahitaji ingawa kuna mambo ya kuongeza ili kupata matokeo mazuri zaidi na kusonga mbele, hata ukiangalia msimu uliopita walifanya vizuri sana katika michuano hii,” amesema Gamondi.