Wakati homa ya pambano la Watani wa jadi ikizidi kupanda, Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamond amesema dakika 130 alizowaangalia Simba zimemtosha kuwasoma na kumpa mwanga wa kufanya maandalizi yake kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa keshokutwa Jumapili (Novemba 05).
Katika mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 11.00 jioni, Young Africans watakuwa wageni.
Akizungumza kambini jijini Dar es salaam, Kocha Gamond amesema amewaangalia wapinzani wake katika michezo miwill anaamini ameyafanyia kazi yote ambayo ameyaona.
“Nimewaangalia Simba SC katika mchezo wao dhidi ya Al Ahly ya Misri na Ihefu nina imani kila nilichowapa nyota wangu watakifanya kwa umakini mkubwa.” amesema
Amesema amefanikiwa kuwasoma wapinzani wao katika michezo miwili ameona ubora na udhaifu wao na kuyafanyia kazi kabla ya kukutana nao mechi inayofuata.
Amesema kubwa ni kufanyia kazi changamoto za timu yake kila idara na kwamba wanapokuwa imara wapinzani wao katika safu ya ushambuliaji na beki imekuwa tatizo kwa kuruhusu bao.
“Itakuwa ni mechi nzuri yenye mbinu na ufundi, tunajiandaa kutafuta ushindi na kujiweka katika nafasi nzuri ya mbio zetu za kutwaa ubingwa wa ligi kuu.” amesema Gamondi
Naye staa wa Young Africans, Maxi Nzengel, amesema hana cha kuwaahidi mashabiki wake kuelekea mchezo huo, anaamini atafanya vyema kwa kushirikiana na wenzake.
Nzengeli ambaye ana mabao matano katika ligi hiyo, amesema ni ngumu kutoa ahadi ya kupachika bao katika kila mchezo lakini anaahidi kuwa atafanya vizuri.
“Ninaamini tutafanya vizuri, mashabiki wetu wanatakiwa kuja kwa wingi kutupa sapoti katika mchezo huu” amesema nyota huyo.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans imeshuka dimbani mara saba ikiwa na alama 18 sawa na Simba SC ambayo imecheza michezo sita.