Kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Namungo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema maandalizi yameenda vizuri malengo makubwa na kuendelea na safari yao ya kukusanya pointi kila mechi kwa ajili ya kutetea ubingwa.
Amesema mechi itakuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu mechi ya duru la kwanza Namungo FC, walionyesha mpira mzuri na kuwapa ushindani mkubwa na kufanikiwa kupata bao dakika za mwisho.
“Tumefanya maandalizi mazuri kukabiliana na Namungo FC, tunawafahamu mechi ya kwanza walitusumbua na sasa tunaingia kivingine kuhakikisha tunavuna pointi tatu ugenini,” amesema kocha huyo.
Alisema hutumia mechi za kuandaa silaha zake ya maangamizi ya robo fainalia ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alisema anafahamu ugumu wa michezo ya kimataifa na kutakiwa kufanya maandalizi kwa kusahihisha makosa yaliyofanyika kwenye michezo ya nyuma.
Ameeleza kuwa licha ya bado hawajajua wanakutana na nani lakini anaimani mechi za ligi zitamsaidia kuandaa kikosi chake vizuri kujiandaa na michezo ya robo fainali.
“Tunajiandaa na mechi za ligi ambazo tutazitumia kutafuta matokeo mazuri kuelekea kuvuna pointi tatu katika kila mechi hizi nne, lakini pia kutumia hizi mechi kujiandaa na robo fainali.
Mechi za makundi zilikuwa ngumu na ushindani mkubwa lakini vijana wamepambana kwa kila hatua na kufanikiwa kufika hatua ya robo kwa kuvuka malengo yetu,” alisema kocha wa Yanga,
Kikosi cha Yanga kimemaliza nafasi ya pili katika Kundi D wakiwa na pointi 8, kimerejea nchini jana kikitokea nchini Misri katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano hiyo dhidi ya Al Ahly inayongoza wakikusanya alama 12.