Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi, Mbrazili mikwara

Gamondi X Robertinho Tanga Gamondi, Mbrazili mikwara

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Novemba 5 saa 11 jioni, Simba na Yanga zitakwaana kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya Ligi msimu huu ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mpaka sasa wanalingana pointi kwenye msimamo huku zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, lakini makocha wa timu hizo, Miguel Gamondi na Roberto Oliveira ‘Robertihno’ wamechimba mkwara mzito kusisitiza ni mechi kubwa na ngumu lakini pointi tatu zipo.

Ingawa Simba wako nyuma kwa mchezo mmoja, rekodi zinaonyesha mara ya mwisho watani hao kukutana Simba iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0, lakini mapema wakati wa ufunguzi wa msimu huu timu hizo zilikutana kwenye Fainali ya Ngao ya Jamii na Simba kushinda tena kwa mikwaju ya penalti 3-1 na kuchukua taji hilo lililokuwa linashikiliwa na Yanga kwa misimu miwili mfululizo.

Kocha wa Simba, Robertinho maarufu kama mtaalam wa soka la malengo ‘Objective football’, ameliambia Mwanaspoti anatambua ubora wa wachezaji wa Yanga kwani ni miongoni mwa timu bora na yenye ushindani hasa kwenye ligi lakini timu yake itakuja kwenye mchezo huo kwa ubora mkubwa.

Robertinho ambaye ni raia wa Brazili mwenye uzoefu na soka la Afrika, alisema endapo wachezaji wake watacheza kwa ubora kama ambavyo walicheza mchezo wa pili wa marudiano dhidi ya Al Ahly ya Misri, hana presha ushindi utakuwa kwao.

Kocha huyo ambaye timu yake haijapoteza mechi yoyote ya ligi msimu huu, alisema kikosi chake sasa kimeiva akiwa na wachezaji wanaoweza kuanza na kutengeneza ushindi pia akiwa na wale ambao wanaweza kuja kuingia na kubadilisha mchezo.

“Yanga wana timu bora lazima uwaheshimu wapinzani wako, ila napata matumaini makubwa zaidi kwani nina wachezaji wenye uzoefu mkubwa, kitu ambacho tutatakiwa kukifanya ni kurudi kucheza kwa ubora kama ambavyo tulicheza kule Misri dhidi ya Al Ahly,” alisema Robertinho ambaye aliwahi kuifunga Yanga akiwa na Vipers ya Uganda.

“Tunatakiwa kutumia nafasi zetu tutakazozitengeneza, mechi kubwa kama hii ya watani haitakuwa na nafasi nyingi sana, lakini kitu kizuri kwa sasa tuna wachezaji ambao wanaweza kuanza na kutengeneza ushindi, pia wapo ambao wanaweza kuingia na kubadilisha mchezo jambo ambalo tumeshafanya huko nyuma.”

Wakati Robertinho akisema hayo, Kocha wa Yanga, Gamondi ambaye ni Muargentina alisema wanakwenda kumalizia maandalizi yao ya mchezo mkubwa ambao uko mbele yao akijua wapinzani wao walimpokonya taji la Ngao ya Jamii.

Alisema ugumu wa mchezo huo utaamuliwa na ubora wa wachezaji jambo ambalo halimpi presha kwani ana uhakika na kikosi alichonacho kipo tayari kwa mechi hiyo kubwa na wachezaji wake wamepania kufanya kila kinachowezekana kupata pointi.

“Ili uwe bora unatakiwa kushinda mechi kubwa na ndogo na huo ni mwendelezo kwani wachezaji wangu wana huo uwezo,” alisema Gamondi ambaye licha ya kutokuwa na straika tegemeo staili yake ya uchezaji imekuwa ikiruhusu kila mchezaji kufunga.

“Simba nawajua nimewaona wakicheza na nimekutana nao pia ila mechi hii itakuwa tofauti kutokana na ugumu wake,” alisema Gamondi ambaye ameipeleka Yanga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka mingi.

“Naamini tutafanya vizuri, tunawaheshimu wapinzani wetu kwani wana wachezaji wenye uzoefu ila timu itakayocheza kwa ubora ndio itakayoshinda, mashabiki wetu waje uwanjani kutekeleza wajibu wao wa kuwapa nguvu wachezaji, sisi tuna timu bora na tunaamini tunaweza kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu kama kila mmoja atafanya majukumu yake ipasavyo.”

Dabi hiyo ambayo Simba ndio mwenyeji inachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya kufanyiwa marekebisho makubwa, mechi hii inatarajiwa kuanza kuanzia saa 11:00 jioni na Mwanaspoti litakuletea kila kitu ‘live’ kupitia kwenye mitandao yetu ya kijamii na gazeti.

Chanzo: Mwanaspoti