Kocha wa Yanga amesema kama kuna mtu anadhani mechi za Mapinduzi ni laini anakosea na kwamba hizo ni ngumu pengine kuliko Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema mechi hizo zina ugumu mkubwa kutokana kwanza ratiba yake kuwa ngumu kwa mechi kuchezwa karibukaribu.
Gamondi alisema hatua ya kucheza mechi kila baada ya siku moja ina ugumu mkubwa ambapo wachezaji wamekuwa hawapati muda wa kutosha wa kupumzika wala kurudisha miili yao sawa.
“Maishani hizi ni mechi rahisi kwa kuwa ni mashindano mafupi hizi ni mechi hatari pengine kuliko zile za Ligi Kuu, kitu cha kwanza kigumu ni hii ratiba yake ukiwa kocha au mchezaji utaelewa kwanini hii ni ratiba ngumu, inakutaka kila baada ya siku moja ucheze mechi na mashabiki wanataka kuona timu inashinda,” alisema Gamondi.
“Wachezaji hawapati muda wa kupumzika vizuri wala kurudisha miili yao sawa, hili linaweza kutengeneza hata majeruhi kama hutakuwa na mabadiliko makubwa ya wachezaji, bahati mbaya haya mambo ya msingi tunatakiwa kuyaona sisi sio watu wengine, huko nje watu wanataka kuona timu inacheza kwa ubora uleule.
“Hata maandalizi yetu kama makocha kuna wakati tunakumbana na changamoto, hupati muda wa kutosha kujiandaa na ubora wa mpinzani wako lakini kwetu tuna furaha tumepata matokeo mazuri kwenye hizi mechi tatu.”
Yanga jana usiku ilitolewa kwenye mashindano hayo na APR ya Rwanda katika hatua ya robo fainali.