Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amekiri kwamba kikosi chake hakijapata muda wa kufanya maandalizi kuelekea mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC kwani ratiba ilikuwa mbaya upande wao.
Gamondi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 6, 2023 jijini Mwanza wakati akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Geita Gold utakaopigwa kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Amesema siyo kwamba wamecheza Mbeya juzi kisha jana wakasafiri mpaka Dar es Salaam, walipofika wakaunganisha usiku kwenda Mwanza hivyo watapumzika leo na kesho watakuwa uwanjani tena..
"Kwanza kabisa mara nyingi kwenye mikutano na wanahabari siulizwi maswali mengi napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wanahabari wajiskie huru kuniuliza swali lolote nipo hapa kwa ajili yao, maana muda pekee ninaongea nao ni kwenye mikutano kama hii.
"Tumepoteza mchezo uliopita dhidi ya Ihefu, lakini mashabiki wameendelea kuwa pamoja nasi na kutupa sapoti kama vile bado hatujapoteza mchezo wowote ni kazi yetu sasa kuhakikisha kwenye mchezo wa kesho tunajitoa kwa nguvu zote kuhakikisha tunapata ushindi.
"Maandalizi kwa upande wetu siyo mazuri sana kutokana na ratiba lakini sisi ni wataalamu na ligi kuna muda inakuwa na ratiba ngumu lazima kuwa tayari. Leo tutakuwa na mazoezi jioni, ambayo yatatusaidia kuona hali ya wachezaji kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya Geita Gold," amesema Gamondi.