Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi, Kouassi wamejipata

Yao Gamondi Gamondi, Kouassi wamejipata

Wed, 23 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi mdogomdogo ameanza kupata rasmi kikosi cha kwanza tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akirithi mikoba ya Nasreddine Nabi.

Gamondi alipopata muda wa kukaa na mastaa wake, mechi yake ya kwanza iliyowatambulisha wachezaji ni dhidi ya Kaizer Chiefs iliyochezwa katika kilele cha Siku ya Mwananchi.

Katika mchezo huo Gamondi alianza na kipa Metacha Mnata, mabeki Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto (nahodha) na Dickson Job.

Viungo walikuwa Jonas Mkude, Max Nzengeli na Mudathir Yahya huku washambuliaji walioanza ni Denis Nkane na Skudu Makudubela.

Wachezaji waliokuwa benchi katika ni Diara Djigui, Abuutwalib Mshery, Yao Attohoula,Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Gift Fred, Zawadi Mauya, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Clement Mzize, Chrispin Ngushi, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Aziz Ki na Pacome Zouazoua.

Gamondi baada ya mchezo alibadili kikosi kwenye mchezo uliofuata uliokuwa wa Ngao ya Jamii (wa kwanza) dhidi ya Azam. Kocha huyo alibakiza wachezaji watano tu walioanza mchezo wa Siku ya Mwananchi ambao ni Mwamnyeto, Nzengeli, Mudathir, Skudu na Kenedy Musonda ambao walichanganywa na wengine sita.

Kocha huyo alifanya mabadiliko kumtoa golini Mnata na kuingia Diara, eneo la beki alitoka Kibabage na Kibwana wakaingia Yao na Lomalisa na kwa Job akaingia Bacca.

Eneo la kiungo alimpumzisha Mkude na Nkane wakaingia Aucho na Farid Mussa na yote ni kuhakikisha anapata kikosi cha kwanza.

Katika mechi hiyo kikosi kilichoanza ni Diara, Yao, Lomalisa, Mwamnyeto, Bacca, Aucho, Maxi, Yahya, Musonda, Farid na Skudu.

Mechi ya pili ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili tu katika kikosi kilichoanza dhidi ya Azam FC.

Wapya walioingia ni Moloko akichukua nafasi ya Skudu na Mzize aliyechukua nafasi ya Farid.

Wakati huohuo, katika mechi hizo mbili Aziz Ki ni mmoja wa wachezaji waliokuwa wanaingia akitokea benchi na alifunga bao kali kwenye mchezo dhidi ya Azam FC. Katika mechi ya hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asas, Gamondi alifanya mabadiliko mengine mawili tu kikosi cha kwanza akimuengua Bacca na kumuanzisha Job pia akimuacha nje Moloko na kuanza na Aziz Ki, aliyeonyesha kiwango bora katika mechi zote alizoingia msimu huu.

Ki kwenye mchezo huo alifunga tena bao na kuonyesha yupo moto msimu huu akipewa nafasi ya kucheza sawa na Musonda.

Katika vikosi vyote ni wazi Gamondi hana shida eneo la kipa kwani Diarra ameshapenya sawa na mabeki Lomalisa, Yao, Mwamnyeto (nahodha) huku Bacca na Job wakipishana.

Upande wa kiungo, Maxi na Mudathir wanaonekana kuanza kujihakikishia namba kwani mechi nne zote tangu Siku ya Mwananchi wapo katika kikosi cha kwanza.

Aucho baada ya mechi ya Siku ya Mwananchi ameanza kikosini mechi zote tatu za mashindano.

Eneo la ushambuliaji mchezaji pekee aliyeanza mechi zote nne ni Musonda na amefunga mabao mawili, moja dhidi ya Kaizer na jingine dhidi ya Asas.

Akizungumzia namna kocha huyo anavyosaka kikosi chake, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hery Morris alisema bado anaendelea kutengeneza kikosi cha uhakika ndio maana wapo wachezaji wanaoingia na kutoka. “Unaweza ukakuta hata hawa ambao wanapewa nafasi ya kuanza leo hii baadaye watakuja kubadilika kutokana na namna ambavyo wengine wataonyesha viwango mazoezini.

“Musonda ni kati ya wachezaji wanaopewa nafasi ya kucheza na anajitahidi kufanya vizuri, mtu kama Aziz Ki alikuwa hapati nafasi lakini juzi tumeona amerejea na kufunga.”

Mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema kocha hafanyi mabadiliko mengi kwenye kikosi kwa sababu wachezaji ni wazuri na wameanza kuingia kwenye mfumo wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live