Kocha mkuu wa kikosi cha Yanga SC, Miguel Gamondi, amezungumzia mchezo wa kesho Ijumaa wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Singida Fountain Gate.
Mchezo huo uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, utaanza majira ya saa 12:15 jioni.
Kuhusu mchezo huo, Gamondi alisema: “Vijana wangu wapo tayari kwa mchezo huu ambao ninatarajia utakuwa mgumu, mara zote tunajaribu kushinda mechi. Naamini kesho tutakuwa na mchezo mzuri.
“Wakati mwingine si rahisi wachezaji kurudi kwenye hali ya kawaida kwa haraka, Jumatatu tulicheza, tunacheza tena Ijumaa, ninajaribu kuchagua wachezaji ambao wanakuwa fiti kulingana na mpinzani wetu.
“Nina furaha na wachezaji nilionao, ninapenda kuwapa nafasi kila mmoja, malengo ni kushinda mechi. Katika kazi yetu, uamuzi huu ni mgumu sana kama kocha.
“Kesho mtaona kikosi cha kwanza, mtaona namna timu itakavyocheza, lakini siku zote tunafanya kazi na wachezaji wote, wanafanya kazi kubwa.”
ANAWAZUNGUMZIAJE SINGIDA “Singida ni timu nzuri, ilicheza vizuri katika mashindano ya Afrika dhidi ya Future, naweza kusema kila timu inayokuja kucheza na Yanga inajipanga kwa sababu misimu miwili Yanga imekuwa bingwa, tunatakiwa kuwa tayari kwa hilo. Ninapenda kucheza mechi za aina hii kwa sababu msisimko wa mashabiki unakuwa mkubwa na kwa wachezaji pia kuonesha viwango bora.
“Singida ya msimu huu ni tofauti na iliyopita, imebadilisha makocha wawili, wana falsafa mpya, ninaamini watakuja na matumaini mapya kujaribu kutufunga. Nimewaambia wachezaji wangu wasahau yaliyopita,” alisema Gamondi