Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa mshambuliaji wake, Joseph Guede ameanza kuimarika baada ya kukizoea kikosi na kuongeza kujiamini na umakini akifika kwenye eneo la mwisho.
Gamondi amesema hayo jana baada ya kumalizika kwa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la NBC dhidi ya Tabora United na kufanikiwa kushinda bao 3-0 katika Dimba la Chamazi huku Guede akifunga bao la 3.
“Ninafuraha kwa kufanikiwa kufuzu kwenda nusu fainali, kiwango kizuri hata kipindi cha kwanza nilikuwa na furaha sana, tulitembeza mpira haraka haraka kama ambavyo tulipanga kufanya. Tlitawala mchezo na kutenegeza nafasi lakini tulitumia moja tukapata bao na hata kipindi cha pili tulikuwa vizuri.
“Kwenye mechi nane za mwisho tumeruhusu bao moja tu dhidi ya Simba, ni jambo zuri hasa mwisho wa msimu.
“Guede ni mchezaji mzuri, kufunga ni suala la muda tu kwa mshambuliaji mzuri. Tulimpa nafasi ya kuzoea mazingira, kuzoea timu na kujiamini, amekuwa akijituma na sasa anafunga tu kila mechi,” amesema Gamondi.
Guede ambaye amesajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la msimu huu mpaka sasa ameifungia Yanga mabao 8.
Guede amefunga mabao mawili dhidi ya Polisi Tanzania (CRDB), bao 1 dhidi ya CR Belouizdad (CAFCL), mabao mawili dhidi ya Singida FG (NBCPL), bao moja dhidi ya Simba Sc (NBCPL), bao moja dhidi ya Coastal Union (NBCPL) na bao moja dhidi ya Tabora United (CRDB).