Yanga imekata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya juzi kuwang’oa Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0, lakini kocha wao Miguel Gamondi amethibitisha kwamba bado kikosi chake kina uhitaji.
Akizungumza Gamondi amesema baada ya kikosi chake kufuzu bado anahitaji maboresho zaidi ya kuongeza watu bora kwenye timu hiyo.
Gamondi alifafanua akisema hatua ambayo Yanga imeingia haitakuwa rahisi ambapo anataka kukiongezea nguvu zaidi kikosi chake kupitia dirisha lijalo la usajili.
“Kufuzu ni hatua moja lakini lazima tufanye tathimini ya kina juu ya kikosi chetu tutakwenda kukabiliana na timu kubwa na ngumu zaidi ambazo zimefuzu kama sisi,” alisema Gamondi.
“Tutaangalia ni namna gani na maeneo gani tutakayoyaboresha baada ya vikao na viongozi wangu wa klabu wakati tunasubiri kujua ni timu zipi tutapangiwa nazo.”
Hata hivyo, Gamondi alisema hatua hiyo itategemea na bajeti ya klabu lakini pia kufanya hesabu sahihi ya wachezaji gani wa kupunguza kwavile tayari Yanga ilishakamilisha idadi ya wachezaji wachezaji wa kigeni kikanuni.
“Kusajili kuna mambo mengi ya kuzingatia ni lazima kwanza tukutane na viongozi. Kuna bajeti inahitajika lakini pia tayari hapa kwetu tuna wachezaji kumi na mbili utaona kwamba lazima Kuna mchakato upite,” alisema.
Ingawa Gamondi hakutaka kuonyesha moja kwa moja lakini taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba kocha huyo bado anasisitiza kuletewa mshambuliaji wa kati mwenye makali ya kujua kufunga.