Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi, Benchikha yeyote aje robo fainali CAF

Benchikha X Gamondi Kimataifa Gamondi, Benchikha yeyote aje robo fainali CAF

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania imeweka heshima katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikiwa ni nchi pekee iliyoingiza timu mbili katika robo fainali na sasa zote zinasubiri kujua zitakutana na nani kwenye hatua hiyo, huku makocha wa timu hizo, Abdelhak Benchikha na Miguel Gamondi wakitamba kwa kujiamini wapo tayari kukutana na yeyote kwani wapo freshi.

Yanga ilitangulia mapema kutinga hatua hiyo wiki iliyopita mbele ya CR Belouizdad ya Algeria iliyoinyoa mabao 4-0 kabla ya Ijumaa iliyopita kukamilisha ratiba ya Kundi D kwa kufungwa 1-0 na vinara wa kundi hilo, Al Ahly ya Misri, wakati Simba ilivuka juzi usiku ilipoifumua Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 6-0 katika mechi ya Kundi B.

Simba imeingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya nne kati ya misimu sita iliyopita ya ikifikisha pointi tisa ikishika nafasi ya pili nyuma ya Asec Mimosas iliyoongoza kundi, ilihali Yanga imefuzu ikivuna pointi nane, ikiwa ndio timu iliyopenya hatua hiyo kwa idadi ndogo ya pointi kulinganisha na wapinzani wengine saba.

Timu hizo zote kwa sasa zinasubiri droo ya hatua hiyo ya robo fainali na zile za nusu fainali pamoja na fainali itakayofanyika wiki ijayo kabla ya mechi za mkondo wa kwanza kuanza kupigwa kati ya Machi 29-30 na zile za marudiano Aprili 5-6, huku kila mmoja ikiwa na uwezekano wa kukutana na Petro Atletico ya Angola na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na zikitofautiana kwa Al Ahly ya Misri na Asec Mimosas zilizokuwa katika makundi yaliyowavusha.

Tuanze na Gamondi wa Yanga, kocha huyo Muargentina ameliambia Mwanaspoti kuwa baada ya kikosi hicho kutinga hatua hiyo kwa sasa wanasubiri kujua wataangukia kwa nani kati ya Mamelodi, Petro Atletico au Asec Mimosas.

Gamondi alisema Yanga haina sababu ya kumuogopa mpinzani yeyote zaidi ya kumheshimu yule ambaye droo itamtaja kuwa atavaana nao basi, wataingia msituni kujipanga kwa ajili ya mechi hizo mbili za nyumbani na ugenini.

“Tulikuwa katika kundi gumu zaidi, niliwahi kuona sehemu watu wakituona kama tusingeweza kuvuka, lakini tuliishi na ubora na hesabu zetu na sasa tuko hapa robo fainali,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Tuna kikosi imara sana, sidhani kama tunastahili kuihofia timu yoyote, kwangu nitaiheshimu timu tutakayopangiwa lakini ili uwe bora na kuthibitisha ubora, tunatakiwa kucheza na walio bora na upambane nao, nadhani Yanga tutakwenda kuonyesha hili, kwa sasa tunarudisha akili kwenye mechi za hapa nyumbani.”

Yanga kwenye mechi sita za Kundi D imeibuka na ushindi mara mbili, ikapoteza pia mbili na kutoa sare mbili vilevile, ikimaliza ya pili ikivuna pointi 8 na mabao tisa ya kufunga na kufungwa sita, wakati watetezi na vinara wa kundi, Al Ahly walivuna pointi 12 katika mechi hizo, wakiwa hawajapoteza hata moja wakishinda tatu na sare tatu pia.

Kwa hesabu ni kwamba Yanga haiwezi kukutana na Al Ahly, lakini itavaana na kinara mmojawapo kutoka kundi A, B na C na itaanzia nyumbani mechi za robo fainali kisha kwenda kumalizia ugenini, japo Gamondi mwanzoni hakutaka hesabu hizo kwa kutambua ugumu wa kumalizia mechi ugenini.

Yanga hii ni mara ya kwanza kutinga hatua hiyo baada ya kupita miaka 25 ilipotinga 8-Bora mwaka 1998 mwaka mmoja baada ya Klabu Bingwa Afrika kubadilishwa kuwa katika mfumo unaotumika sasa, lakini ikiwa na kumbukumbu nzuri ya msimu uliopita ilipotinga hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika na kupenya hadi fainali.

Wakati Gamondi akiyasema hayo, kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alisema kiwango kilichoonyeshwa na kikosi hicho juzi usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kulazimisha matokeo yaliyowavusha robo fainali dhidi ya Jwaneng Galaxy iliyoifumua mabao 6-0 ni ishara kwamba kimeanza kuimarika.

Benchikha alisema wakati wakisubiri droo hiyo itakayowakutanisha dhidi ya timu moja kati ya Petro, Mamelodi na Ahly, amewataka wachezaji wa kikosi hicho kujipanga kurudia kiwango hicho kwenye mechi za hatua inayofuata.

“Mimi sio kocha wa kuogopa wapinzani, wakati tunajiandaa kukutana na Galaxy, niliambiwa waliwahi kuifunga Simba hapa kwa mabao 3-1, lakini niliwambia wachezaji wanatakiwa kucheza mechi hii (dhidi ya Galaxy) kwa akili kubwa,” alisema Benchikha na kuongeza;

“Tukijua tutakutana na nani tutakuwa na mpango maalum wa kucheza hizo mechi mbili ili tushinde, nadhani kitu bora zaidi ni kwa wachezaji, wanatakiwa kuhakikisha tunaendelea kucheza kwa ubora kama huu, kuwa na nidhamu kubwa kuanzia nyuma, katikati na kule mbele tufunge zaidi.”

Ushindi huo wa Simba uliifanya kumaliza nafasi ya pili ya kundi hilo kwa kufikisha pointi tisa, kutokana na kushinda mechi mbili kutoka sare tatu na kupoteza moja, ikifunga mabao tisa na kufungwa mawili tu, wakati Asec ilimaliza kama kinara kwa pointi 11.

Hii ni robo fainali ya tano ndani ya misimu sita kwa Simba katika michuano ya CAF tangu 2018-2019 zikiwamo nne za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho na mara zote ilikwama hapo ikichemsha mbele ya wapinzani na safari hii wakiwa na mtihani wa kuvunja mwiko wa kutovuka hatua hiyo kwenda nusu fainali.

Mwaka 2018-2019 ilizuiwa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1, kisha msimu uliofuata ilitolewa raundi ya awali kabla ya kurejea tena 2020-2021 ilipotolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa kipigo cha 4-3 na msimu uliofuta wa 2021-2022 ilicheza robo ya Kombe la Shirikisho la kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Orlando iliing’oa Simba kwa penalti 4-3 baada ya matokeo ya 1-1.

Chanzo: Mwanaspoti