Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gamondi, Aziz Ki wajifungia robo saa

Aziz Ki Gamondi Yanga 1024x926 Gamondi, Aziz Ki wajifungia robo saa

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga tayari ipo jijini Dar es Salaam ikitokea Morogoro ilikoenda kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC na kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, huku kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi akisema hiyo ndio Yanga aliyoitaka kisha kujifungia kwa robo saa na Stephane Aziz Ki ili kuyajenga kambini.

Ushindi huo wa Yanga umeifanya timu hiyo kuzidi kujikita kileleni ikifikisha pointi 43 kutokana na mechi 16 na sasa inajiandaa kushuka uwanjani kesho Jumanne kucheza mechi ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Polisi kabla ya kuikabili CR Belouizdad ya Algeria wikiendi hii katika mechi ya raundi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya ushindi huo uliotokana na mabao matatu kutoka kwa viungo washambuliaji, Mudathir Yahya aliyefunga mawili na jingine la Pacome Zouzoua na kuwafanya kila mmoja kufikisha jumla ya mabao sita katika msimu huu, kocha  Gamondi ametoa tamko kwamba, kiwango ambacho timu yake ilikionyesha ndio njaa ya ushindi ambayo anaitaka timu yake irudi kuiendeleza kwenye mechi mbalimbali inazoshiriki.

Kocha huyo alisema licha ya ushindi huo, bado anaamini Yanga ingeweza kushinda kwa idadi kubwa ya mabao endapo tu washambuliaji wa timu hiyo wangekuwa na utulivu wanapofika eneo la mwisho la kushambulia, kwani walitengeneza nafasi nyingi zilizopotezwa kwa kukosa umakini.

“Hiki ndio kiwango ambacho tulikuwa nacho kabla ya Ligi kusimama, naona tunaanza kurejea kule ambako tulikuwa tunacheza, tunatakiwa kuwa na njaa ya ushindi kama hivi ambavyo tulicheza jana (juzi),” alisema Gamondi na kuongeza;

“Nawaheshimu sana wapinzani wetu, narudia hii (KMC) ni timu ambayo inanivutia inavyocheza kwa wachezaji wao kujiamini sana, lakini kama tungekuwa na utulivu tungeweza kushinda zaidi ya mabao kama haya, kitu muhimu tunatakiwa kuendeleza njaa ya ushindi mkubwa.”

Kabla ya ushindi huo ambao uliwakuna mashabiki na wapenzi wa timu hiyo, Yanga ilirudi katika Ligi Kuu kwa kulazimishwa suluhu na Kagera Sugar, kisha kushinda bao 1-0 kwa mbinde mbele ya Dodoma Jiji na kuzifunga Mashujaa na Tanzania Prisons kwa kutokwa jasho kwelikweli tofauti na mechi hiyo ya KMC iliyopigwa Moro.

GAMONDI NA AZIZ Kama hujui, mara baada ya mchezo huo wa juzi kinara wa mabao katika Ligi Kuu na Yanga kwa sasa, Stephanie Aziz KI ambaye alionekana kama hakufurahia kutolewa uwanjani, kocha huyo aliamua  kufanya naye kikao kifupi cha muda wa kama dakika 15 ambacho pia baadaye kiliwahusisha vigogo wa klabu hiyo.

Kocha Gamondi alifichua aliamua kufanya kikao hicho na Aziz KI kwa lengo la kumtuliza presha aliyoonekana kuwa nayo tangu akiwa uwanjani na hata alipokuwa akifanyiwa mabadiliko na kukiri hana shida na kiungo mshambuliaji japo anajua hakufurahia kutolewa kwa vile anataka kufunga mabao zaidi.

“Hakuna tatizo lolote, Aziz alitaka aendelee kubaki uwanjani ili afunge zaidi, ni sawa...lakini sisi tuliona kitu zaidi ya hapo jambo zuri ni kwamba yuko sawa na nimezungumza naye na kuweka kila kitu na mambo yapo sawa,” alisema Gamondi, kocha aliyeajiriwa akitokea Argentina.

Kocha huyo alisema kwa mchezaji mwenye kiu kubwa ya mafanikio, huwa na tabia ya kutopenda kubadilishwa uwanjani sio kwa Tanzania tu, bali hata kwingineko, ndio maana aliamua kukaa naye kuzungumza ili kutambua kama mchezaji lazima ajue timu inahitaji matokeo mazuri ya kuibeba kwenye mbio za ubingwa.

Yanga ndio mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu wakiwa wanashikilia mataji 29 na sasa wanatetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo, wakiiacha Simba iliyopo ya pili kwenye msimamo kwa pointi saba, japo ina mchezo mmoja mkononi, huku Azam iliyokuwa inaongoza ligi kwa muda mrefu ikiwa na alama 35 na leo inashuka uwanjani kucheza na Tabora United.

Chanzo: Mwanaspoti